NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Ligi Kuu Tanzania Bara inaendelea leo kwa michezo minne yenye ushindani mkubwa, huku vita ya kusaka pointi tatu ikitarajiwa kuwa kali katika viwanja mbalimbali nchini. Miongoni mwa michezo inayosubiriwa kwa hamu kubwa ni pambano kati ya Mashujaa dhidi ya Simba.

Mapema saa 8:00 mchana kutakuwa na michezo miwili, ambapo Mtibwa Sugar itaikaribisha KMC, huku Tanzania Prisons ikiwa mwenyeji wa Fountain Gate. Baadaye, Simba itashuka dimbani kuvaana na Mashujaa kabla ya Azam FC kuhitimisha ratiba ya siku kwa kuwakaribisha Pamba Jiji.

Macho na masikio ya wadau wengi wa soka yataelekezwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, kuanzia saa 10:15 jioni ambapo Mashujaa watawakaribisha Simba katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na ubora wa timu hizo mbili msimu huu.

Simba itaingia uwanjani ikimtegemea mshambuliaji wake kinara, Seleman Mwalimu, ambaye anaongoza kwa mabao ndani ya kikosi hicho akiwa nayo saba. Kiungo mshambuliaji Clatous Chama pia atakuwa mchezaji wa kuangaliwa baada ya kurejea kwenye kiwango bora kwa kufunga mabao matatu katika michezo mitatu iliyopita.

Wekundu hao wa Msimbazi watakuwa na morali ya rekodi nzuri dhidi ya Mashujaa, kwani katika michezo mitano ya ligi iliyopita iliyowakutanisha, Simba imeshinda yote, ikifunga mabao manane na kuruhusu bao moja pekee

Hata hivyo, Mashujaa inayofundishwa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ imekuwa ngumu kufungika nyumbani msimu huu, ikishinda michezo minne na kutoka sare saba katika mechi zake za nyumbani.

Akizungumzia mchezo huo, kocha wa Simba, Steve Barker, amesema anatarajia upinzani mkubwa kutoka kwa Mashujaa kutokana na uimara wao wanapocheza nyumbani, lakini ana imani kikosi chake kiko tayari kutekeleza mpango wa ushindi.

“Nilitazama mechi yetu ya mwisho dhidi yao, ilikuwa ngumu sana. Ninaamini hata safari hii haitakuwa rahisi kwa sababu ni timu inayocheza kwa ushindani mkubwa ikiwa nyumbani,” alisema Barker.

Kwa upande wa Mashujaa, uimara wa safu yao ya ulinzi nyumbani umekuwa moja ya silaha kubwa msimu huu, jambo ambalo Simba italazimika kutafuta mbinu za kulivunja.

Katika michezo mitano iliyopita, Mashujaa haijapoteza hata mmoja, ikitoa sare nne na kupata ushindi mmoja dhidi ya TRA United kwa bao 1-0.

Tangu Julio achukue mikoba ya kuinoa timu hiyo kutoka kwa Salum Mayanga, Mashujaa haijapoteza mchezo wowote, huku ikifanikiwa kufunga mabao mawili katika michezo mitano ya mwisho.

Kwa sasa Mashujaa inashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 26, baada ya kufunga mabao 11 na kuruhusu mabao 19 kabla ya michezo ya jana.

Simba pia italazimika kuwa makini na safu ya ushambuliaji ya Mashujaa inayowaongoza Jafary Kibaya aliyefunga mabao mawili pamoja na Ismail Mgunda mwenye bao moja dhidi ya TRA United, kwani wakipewa nafasi wana uwezo wa kuleta madhara langoni.