Mchezo wa Dabi ya Kariakoo katika Ligi Kuu Bara uliomalizika kwa sare ya 2-2, umeiletea Yanga maumivu makali ikipgwa faini ya Sh30 milioni huku maafisa wake wawili wakikumbana na adhabu za kusimamishwa.
Taarifa iliyotolewa na Kamati ya Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Tanzania, imesema katika mchezo huo wa Mei 3, 2026 dhidi ya Simba, Yanga imepigwa faini ya Sh30 milioni kwa kosa la kukataa kutumia chumba rasmi cha kuvalia kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
Kwenye tukio hilo, Yanga ilitumia nyumba iliyo nje ya uwanja upande wa pili wa barabara kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
