cha no 656 na 654 Mkuu wa kitengo cha upasuaji katika Hospitali ya mialinga, ameiomba Serikali Iboreshe barabara ya Mbinga

………..

Na Mwandishi Wetu, Mbinga

BAADHI ya wakazi wa wilaya ya Mbinga na Nyasa Mkoani Ruvuma, wameipongeza Hospitali Litembo inayomilikiwa na kanisa katoliki jimbo la Mbinga kwa kuboresha huduma zake hasa ya upasuaji na huduma ya mama na mtoto.

Wamesema,maboresho makubwa ya miundombinu na vifaa tiba yameleta matokeo chanya kwa kuwa wanapata huduma mapema zaidi kutoka kwa wataalam wabobezi wenye uwezo wa kutoa huduma mbalimbali za afya ikilinganisha na hospitali nyingine mkoani Ruvuma.

Elizaberth Kapinga mkazi wakijiji cha Maguu wilayani Mbinga alisema,huduma za mama na mtoto katika hospitali hiyo ni nzuri,hata hivyo ameshauri uongozi wa hospitali kuendelea kuleta vifaa tiba na kuwaongezea ujuzi zaidi watumishi wake ili kuimarisha huduma za afya kwa wagonjwa.

“Katika hospitali hii huduma ni bora na tunahudumiwa vizuri,tunalipongeza kanisa katoliki jimbo la Mbinga kwa maono ya kuanzisha hospitali hii ambayo ni msaada mkubwa kwetu sisi wananchi wa kipato cha chini,inatusaidia kupunguza gharama ya kusafiri kwenda wilaya nyingine za mkoa wa Ruvuma mikoa mingine hapa kufuata huduma za kibingwa”alisema Komba.

Jane Matembo mkazi wa kijiji cha Kitula,amepongeza kazi nzuri ya kuhudumia wagonjwa inayotolewa kwa gharama nafuu na kueleza kuwa,hali hiyo inatokana na uwepo wa madaktari na wauguzi waliofanya kazi kwa muda mrefu wanaofahamu namna ya kutoa huduma za uzazi kwa kufuata maadili na miiko ya taaluma.

“Hospitali ya Litembo ipo umbali wa kilometa 28 kutoka Mbinga mjini ambako kuna hospitali ya wilaya Mbuyula,lakini tunashukuru sana kupata huduma bora za mama na mtoto katika hospitali hii,kwani tunapopata ujauzito tunakimbilia hapa ili kupata huduma kwani kuna wataalam wengi na wenye ujuzi mkubwa zaidi”alisema Matembo.

John Kapinga mkazi wa Nyasa ambaye alikutwa na mwenzi wake kwenye kliniki ya mama na mtoto,ameipongeza hospitali ya Litembo kwa kutoa elimu inayowasaidia kufahamu lishe ya mama mjamzito,dalili za hatari na maandalizi ya kujifungua kwa wajawazito.

“Tunawashukuru wafanyakazi wa hospitali hii kutushawishi hata sisi wanaume kufika na kupewa elimu ya malezi ya mama mjamzito na mtoto mchanga,hii inaturahisishia kufahamu mapema kama kuna changamoto na kuja kumuona Daktari,ninatarajia kupata mtoto wa pili na tangu nianze kupata huduma katika hospitali hii sijawahi kupata changamoto yoyote”alisema Kapinga.

Mkurugenzi wa hospitali ya Litembo Padri Raphael Ndunguru alisema,huu ni mwaka wa 65 tangu hospitali hiyo ilipoanzishwa mwaka 1961 na sasa iko ngazi ya wilaya(District level),ambapo ameishukuru serikali kuboresha huduma za afya ikiwemo kuanzisha zahanati,vituo vya afya na hospitali.

Alisema,kwa sasa wanafikiria hospitali hiyo kupanda ngazi kuwa hospitali ya mkoa na wameshaanza mkakati kuhakikisha mpango wao unakamilika ili kuwezesha kutoa huduma nyingi na kubwa zaidi za afya kwa ngazi ya mkoa.

Alisema, kazi kubwa inayofanyika katika hospitali ni kuboresha mindombinu iliyopo kwa kujenga mochwari kubwa,jengo la dharura,jengo la utawala,kuweka vifaa tiba vya kisasa kama CT Scan na katika kipindi hiki cha maandalizi hayo tayari kuna madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani,upasuaji na magonjwa ya uzazi na akina mama.

“Hawa tayari ni uwekezaji mkubwa ikiwa ni maandalizi ya mpango wa kupanda ngazi hospitali yetu kutoka ngazi ya wilaya na kuwa ya mkoa,tunakosa daktari bingwa wa magonjwa ya watoto hivyo tukiwa na madaktari bingwa watano na miundombinu tunayoweka na huduma za kibingwa tutafikia level ya hospitali ya mkoa”alisema Padri Ndunguru.

Amewataka wananchi wa wilaya ya Mbinga,mkoa wa Ruvuma na mikoa mingine hapa nchini kutumia hospitali ya Litembo kupata huduma za afya na kuwa na mazoea ya kufanya uchunguzi wa afya zao ili kupata huduma mapema na kuokoa maisha yao.

Kwa upande wake Muuguzi kiongozi kitengo cha upasuaji kwa wanawake Petronia Kalinga alisema, kuna mabadiliko makubwa kiutendaji kwa watumishi na uboreshaji wa miundombinu ambazo zimewezesha madaktari na wauguzi kutoa huduma bora kwa wagonjwa wanaofika kupata matibabu.

“Katika hospitali yetu mazingira ya kazi yameboreshwa na yanaendelea,hiyo ni hatua kubwa sana,vitendea kazi ni vingi na hata visipokuwepo tukiomba tunapata kwa wakati,maboresho yanayofanyika yanatusaidia kutoa huduma kwa haraka na kuleta ufanisi kwa wagonjwa wetu”alisema Kalinga.

Kalinga,amelipongeza kanisa katoliki Jimbo la Mbinga kuanzisha hospitali hiyo,kwani kama isingekuwepo wananchi hasa wenye kipato cha chini wangepata shida kwenda mbali na maeneo yao kufuata huduma za afya.

“Wagonjwa wanakuja Litembo kwa sababu wanafahamu kuna huduma bora,tuna upongeza uongozi wa hospitali kwa kuongeza watumishi wakiwemo madaktari bingwa wa vitengo mbalimbali”alisema. wito kwa watu wanaohitaji huduma za upasuaji wafike Litembo ili wapate huduma za uhakika.