Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya familia ya jeshi la polisi
Na Hellen Mtereko,Mwanza
MKUU wa mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amelipongeza Jeshi la Polisi mkoani humo kwa namna wanavyoimarisha Ulinzi na Usalama.
Mtanda ameyasema hayo leo Jumamosi Mei 9 katika maadhimisho ya Siku ya Familia ya Jeshi la Polisi yaliyofanyika katika uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza.
Maadhimisho hayo ya Siku ya Familia ya Jeshi la Polisi yamelenga kuimarisha mshikamano kati ya askari polisi, familia zao pamoja na wananchi, sambamba na kutambua mchango wa jeshi hilo katika kudumisha amani na usalama nchini.
Mtanda, amelipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya katika kuhakikisha amani, utulivu na usalama vinavyoendelea kuimarika ndani ya mkoa huo.
Amesema kuwa kazi inayofanywa na askari wa jeshi hilo imekuwa chachu ya maendeleo kutokana na wananchi kuendelea kufanya shughuli zao za kiuchumi katika mazingira salama na yenye utulivu.
Amesema serikali inatambua mchango mkubwa wa Jeshi la Polisi katika kulinda raia na mali zao, huku akiwasisitiza askari kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo mkubwa kwa taifa.
“Jeshi la Polisi limeendelea kufanya kazi nzuri ya kuimarisha ulinzi na usalama, Serikali inatambua na kuthamini juhudi zinazofanywa na askari wetu katika kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na usalama wakati wote,” Amesema Mtanda.
Amesema serikali ya awamu ya sita imeendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa askari polisi nchini kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vituo vya polisi, nyumba za askari pamoja na kuongeza vitendea kazi vya kisasa.
Ameeleza kuwa hatua hizo zina lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi ndani ya Jeshi la Polisi na kuwawezesha askari kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uharaka zaidi.
“Serikali imeendelea kupandisha vyeo askari, kujenga vituo vya polisi na nyumba za askari pamoja na kuongeza vitendea kazi kama magari na vifaa mbalimbali vya kiutendaji ili kuhakikisha jeshi linafanya kazi katika mazingira bora,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Mtanda amewataka wananchi kuendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi kupitia Kamisheni ya Polisi Jamii ili kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya uhalifu.
Amesema ushirikiano kati ya polisi na wananchi ni nguzo muhimu katika kudhibiti uhalifu na kutoa taarifa za wahalifu kwa wakati.
Aidha, Mtanda amegusia changamoto ya uhalifu wa mitandao na kueleza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuimarisha mifumo ya uchunguzi wa kisasa ili kukabiliana na wahalifu wanaotumia teknolojia kufanya uhalifu.
Amesema maendeleo ya teknolojia yameleta manufaa makubwa lakini pia yameongeza aina mpya za uhalifu, hivyo kuna haja ya vyombo vya usalama kwenda sambamba na mabadiliko hayo ya kidijitali.
Mtanda amesema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha uwezo wa askari katika matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kusaidia uchunguzi wa makosa ya jinai na kudhibiti uhalifu wa mitandao.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, amesema mkoa wa Mwanza unaendelea kuwa katika hali ya utulivu kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Jeshi la Polisi, wananchi pamoja na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya taaluma, uwajibikaji na haki ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kiusalama.
Amesema Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na jamii katika kutatua changamoto mbalimbali za kiusalama ili kuhakikisha
wananchi wanaendelea kuishi kwa amani na kufanya shughuli zao za maendeleo bila hofu.
