Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) pamoja na wadau mbalimbali wameshiriki mjadala wa jopo la meza ya duara uliofanyika katika siku ya mwisho ya utekelezaji wa Mradi wa BREEDIME, kwa lengo la kutathmini mafanikio, ubunifu na uendelevu wa taasisi uliopatikana kupitia mradi huo.

Mjadala huo uliwakutanisha washirika wa muungano wa mradi pamoja na wadau muhimu kutoka taasisi za afya, udhibiti wa dawa na utafiti, ambapo walijadili athari za mradi katika kuimarisha mifumo ya udhibiti na utayari wa kukabiliana na dharura za afya ya umma.

Katika kikao hicho, washiriki walifanya mijadala ya kina kuhusu namna ya kusambaza matokeo ya mradi kupitia machapisho mbalimbali ya kitaalamu, mikakati ya kuhakikisha uendelevu wa matokeo yaliyopatikana pamoja na mwelekeo wa baadaye wa ushirikiano kati ya taasisi husika.

Washiriki walieleza kuwa mradi wa BREEDIME umeonesha ufanisi mkubwa katika kufanikisha malengo na matokeo yaliyopangwa, huku ukiendelea kuwa na mchango muhimu katika kukidhi mahitaji ya mifumo ya udhibiti wa dawa na vifaa tiba.

Aidha, ilielezwa kuwa matokeo ya awali ya mradi yanaashiria mafanikio makubwa katika kuimarisha uwezo wa taasisi mbalimbali, ingawa uendelevu wake utategemea namna taasisi zitakavyoendelea kuupa kipaumbele na kutoa ushirikiano wa muda mrefu.

Kwa ujumla, wadau walikubaliana kuwa Mradi wa BREEDIME umeweka msingi imara wa kuboresha mifumo ya udhibiti na kuimarisha utayari wa kukabiliana na dharura za afya ya umma Tanzania Bara, Zanzibar na Rwanda.

Miongoni mwa taasisi zilizoshiriki ni TMDA⁠, Karolinska Institutet, Kilimanjaro Clinical Research Institute – KCRI, Muhimbili University of Health and Allied Sciences, Zanzibar Food and Drug Agency – ZFDA⁠, National Institute for Medical Research, Rwanda Food and Drugs Authority pamoja na University of St Andrews.