Na John Bukuku, Dar es Salaam
Benki ya Ushirika Tanzania (Coop Bank) imeendelea kuonyesha mafanikio makubwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake, huku ikitangaza ukuaji wa kasi katika maeneo mbalimbali ya kifedha na kiutendaji, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuchochea uchumi jumuishi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika tawi jipya la benki hiyo lililopo Morocco jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo, Bw. Godfrey Ngula, alisema taasisi hiyo imepiga hatua kubwa katika kujenga msingi imara wa utoaji huduma za kifedha kwa Watanzania wengi, hususan wale waliokuwa nje ya mfumo rasmi wa kibenki.
Alisema kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, mizania ya benki imekua kwa asilimia 281 kutoka Sh. bilioni 46 mwaka 2025 hadi kufikia Sh. bilioni 178, hali inayoonesha kasi kubwa ya ukuaji wa taasisi hiyo ndani ya muda mfupi.
Aidha, kitabu cha mikopo kimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 56, kutoka Sh. bilioni 16 hadi kufikia zaidi ya Sh. bilioni 101, hatua inayodhihirisha kuongezeka kwa imani ya wateja pamoja na kupanuka kwa huduma za kifedha zinazotolewa na benki hiyo.
Kwa upande wa amana za wateja, benki imefanikiwa kuongeza kwa zaidi ya asilimia 700, kutoka Sh. bilioni 12 hadi kufikia zaidi ya Sh. bilioni 101, ikiwa ni matokeo ya mikakati madhubuti ya kuvutia wateja na kuhamasisha matumizi ya huduma za benki.
Katika mapato, benki imerekodi ongezeko kubwa ambapo mapato yatokanayo na riba yameongezeka kwa asilimia 938 huku mapato yasiyo ya riba yakifikia Sh. bilioni 2.1 kutoka kiwango cha chini mwaka uliopita, hali iliyochangia benki kupata faida ya Sh. milioni 148 kabla ya kodi katika robo ya kwanza ya mwaka huu.
Vilevile, thamani ya fedha za wanahisa imeongezeka kwa asilimia 54 kutoka Sh. bilioni 27 hadi Sh. bilioni 42, huku ubora wa mikopo ukiendelea kubaki imara kwa kiwango cha mikopo chechefu kushuka hadi asilimia 1.08 kutoka asilimia 2 hapo awali.
Katika kuboresha huduma, benki imewekeza kwa kiasi kikubwa katika teknolojia ya kidijitali ikiwemo uzinduzi wa huduma ya simu ya mkononi ya Co-op Pesa pamoja na huduma ya mtandao ya Co-op Net, ambazo zimeongeza urahisi wa miamala na kupanua wigo wa huduma kwa wateja.
Kupitia majukwaa hayo ya kidijitali, benki imeweza kufikia wateja wengi zaidi hata katika maeneo ambayo haina matawi, huku ikitumia mtandao wa mawakala kupitia vyama vya ushirika zaidi ya 64 pamoja na AMCOS na SACCOS nchini.
Katika sekta ya kilimo, benki imefanikiwa kuchakata malipo ya mazao mbalimbali ikiwemo Korosho, Ufuta na Kahawa, ambapo zaidi ya Sh. bilioni 50 zilipitishwa kwa malipo ya ufuta na zaidi ya Sh. bilioni 2 kwa Korosho pekee katika kipindi cha mwaka mmoja.
Ngula alieleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na mkakati wa kulenga sekta ya kilimo ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania, huku benki ikitoa mikopo kwa riba nafuu ya kati ya asilimia 9 hadi 10 ili kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji.
Kwa upande wa upanuzi wa huduma, benki imeongeza matawi kutoka manne hadi saba ndani ya mwaka mmoja, ikiwa ni pamoja na matawi ya Dar es Salaam, Mtwara, Tabora, Kagera na mipango ya kufungua matawi Mwanza na Arusha hivi karibuni.
Aliongeza kuwa benki inalenga kuwafikia Watanzania wasiopungua milioni 10 ndani ya miaka mitano ijayo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ujumuishi wa kifedha kutoka asilimia 22 ya sasa hadi kufikia angalau asilimia 50.
Katika hatua nyingine, benki imejiunga na taasisi ya kimataifa ya ushirika (International Cooperative Alliance), jambo linaloipa fursa ya kupanua ushirikiano kimataifa na kuimarisha nafasi yake katika sekta ya fedha.
Ngula alihitimisha kwa kusema kuwa benki hiyo imejipanga kujenga mfumo imara wa kifedha unaolenga ustawi wa pamoja wa Watanzania, huku ikiendelea kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha inachangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa taifa




