Na Mwandishi Wetu, Tunduru
CHAMA cha walimu Tanzania(CWT)kupitia kitengo cha walimu wanawake wilayani Tunduru Mkaoni Ruvuma,kimeipongeza Serikali kuboresha mazingira ya kazi ikiwemo ujenzi wa miundombinu bora ya madarasa,matundu ya vyoo,maabara na nyumba za walimu ambazo zimepunguza changamoto katika ufundishaji na makazi kwa baadhi ya walimu.
Katibu wa kitengo cha wanawake wa chama cha walimu Tanzania(CWT) wilaya ya Tunduru Evodia Makothaamesema hayo jana,kwenye maadhimisho ya usiku ya walimu wanawake(Women Teachers Night Gala)yaliyofanyika katika ukumbi wa Sky Way Tunduru mjini.
Alisema,chama cha walimu kupitia kitengo cha walimu wanawake,wameandaa sherehe za usiku wa walimu wanawake gala ili kuwakutanisha pamoja walimu wote wanawake ambao ni wanachama wa chama cha walimu Tanzania(CWT)wilaya ya Tunduru ili kushiriki shughuli mbalimbali zitakazowaondolea walimu mfadhaiko katika utendaji wa majukumu yao.
Makotha,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuboresha stahiki za walimu ikiwemo nyongeza za mishahara,kupandishwa madaraja,kulipa stahiki za uhamisho,matibabu na nauli,kuongezeka kwa walimu wanawake katika nafasi za uongozi wa shule kama wakuu wa shule za msingi,sekondari na maafisa elimu kata.
“Ongezeko la fursa katika elimu,sasa tuna fursa nyingi kuliko wakati mwingine wa kutumia teknolojia katika kujifunza na kufundishia kwani mifumo wa TEHAMA kwa sasa ni hadithi kwa walimu”alisema Makotha.
Alisema,licha ya mafanikio hayo bado walimu wanawake wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo msawazo wa majukumu ya ualimu shuleni na ya kifamilia nyumbani ambayo wakati mwingine inawakwamisha katika utendaji wao wa kazi.
Makotha alisema,baadhi ya walimu wanawake hasa wanaoishi na kufanya kazi maeneo ya vijijini wana changamoto kubwa ya nyumba bora za kuishi,kukumbana na unyanyasaji wa kijinsia,hivyo kupelekea kudunisha utendaji wa kazi zao.
Ameishauri Serikali,kuendelea kujenga nyumba nyingi na za kisasa kwa walimu ili kuwaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu na kulinda hadhi ya mwalimu na usalama wao kwani baadhi ya walimu wanaishi hasa wa vijijini wanaishi kwenye nyumba ambazo hazina sifa ya kuishi mtumishi wa umma.
“Baadhi ya shule miundombinu yake sio rafiki,tunakuomba kama kiongozi namba moja wa wilaya yetu usimamie matengenezo ya miundombinu bora shuleni,tunakuhakikishia samani zake zinapatikana zikiwa katika ubora”alisema Makotha.
Ameiomba Serikali,kuwawezesha walimu wanawake mikopo nafuu inayotolewa kupitia idara ya maendeleo ya jamii kwenye Halmashauri za wilaya kwani itawasaidia kujikwamua na umaskini.
Mjumbe wa kamati ya utendaji Taifa ya Chama cha walimu Tanzania(KUT) Sabina Lipukila,amewataka walimu kuendelea kujiunga na chama cha walimu Tanzania(CWT)ili waweze kusaidiwa pale wanapopata matatizo ya kiutumishi ikiwemo stahiki zao na matatizo mengine yaliyopo katika jamii.
“Inawezekana walimu wanakimbilia vyama vingine kwa sababu ya kuangalia makato ya Shilingi elfu tano,lakini wanashindwa kujua ela hiyo inakwenda kufanya kitu gani kwani hauwezi kuendesha chama kwa makato ya shilingi elfu tano,kazi ya vyama vya wafanyakazi hasa chama cha walimu Tanzania ni kutetea wanachama wake”alisema Lipukila.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Denis Masanja,chama cha walimu Tanzania(CWT)ni kiunganishi kati ya walimu na Serikali yao hali iliyopelekea kupata ufanisi mkubwa katika sekta ya elimu hapa nchini.
Alisema,kupitia mahusiano mazuri na mazungumzo ya mara kwa mara kati ya walimu na Serikali mambo mbalimbali yamefanyika na kuzaa matunda kama vile kuboresha miundombinu mbalimbali mashuleni,kuboresha maslahi ya walimu na kulipa malipo ya uhamisho,matibabu na likizo kutolewa kwa wakati.
“Licha ya mafanikio haya baadhi ya walimu wanajitoa katika chama cha walimu Tanzania(CWT) na kujiunga na vyama vingine na wengine hawana chama,nawaomba sana walimu waliojitoa CWT,kuacha kuangaika badala yake walirudi kwenye chama chao kwa mustakabali wa sekta ya elimu katika wilaya ya Tunduru,siku zote umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu”alisisitiza Masanja.





