Na John Bukuku , Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Tukai Mavere, amesema taasisi hiyo imeendelea kuboresha mfumo wa ununuzi wa dawa na bidhaa za afya kwa kuzingatia mikataba ya muda mrefu pamoja na ushirikiano wa karibu na wazalishaji wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari katika kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita, Mavere alisema mfumo huo unalenga kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa dawa, kupunguza gharama na kuongeza uwazi katika mchakato wa ununuzi.
Alisema MSD imeweka mkazo katika matumizi ya mikataba ya muda mrefu (Framework Agreements) inayotekelezwa kupitia mfumo wa kielektroniki wa ununuzi (NeST), ambapo wazabuni huchaguliwa na kuthibitishwa sifa zao, masharti na bei kwa kipindi cha hadi miaka mitatu.
“Mfumo huu unarahisisha upatikanaji wa dawa kwa haraka kwani wasambazaji tayari wanakuwa wamekidhi vigezo vyote, hivyo kupunguza muda wa ununuzi na ucheleweshaji usio wa lazima,” alisema Mavere.
Aliongeza kuwa kupitia mikataba hiyo, MSD inapunguza gharama za matangazo ya zabuni yanayojirudia, huku bei zikibaki thabiti katika kipindi chote cha mkataba, jambo linalorahisisha upangaji wa bajeti.
Kwa mujibu wa Mavere, ununuzi wa bidhaa za afya ni moja ya majukumu makuu ya MSD, ambapo kwa sasa zaidi ya asilimia 80 ya bidhaa hizo huagizwa kutoka nje ya nchi, huku jitihada zikiongezwa kuimarisha ununuzi kutoka kwa wazalishaji wa ndani.
Alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026, MSD inatarajia kuwa na jumla ya bidhaa za afya 1,725, ambapo kati ya hizo, bidhaa 1,354 sawa na asilimia 78.5 zina mikataba ya muda mrefu.
“Katika mikataba hiyo, asilimia 76.5 ni ya wazalishaji moja kwa moja, huku nyingine zikiwa kupitia wasambazaji walioidhinishwa na wazalishaji (authorized dealers),” alifafanua.
Mavere alisema MSD pia imeendelea kuongeza ununuzi kutoka kwa wazalishaji wa ndani, hatua inayolenga kuimarisha viwanda vya ndani, kupunguza matumizi ya fedha za kigeni na kuongeza ajira.
Alibainisha kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026, ununuzi kutoka kwa wazalishaji umefikia asilimia 62, huku baadhi ya bidhaa muhimu kama za saratani zikifikia asilimia 61 na za kisukari asilimia 93 kutoka kwa wazalishaji.
Aidha, alisema MSD imeingia mikataba na viwanda 12 vya ndani vinavyozalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo dawa, majitibabu (intravenous fluids), vitakasa na sabuni za afya, huku viwanda saba vya vifaa tiba navyo vikiwa katika mikataba hiyo baada ya bidhaa zao kusajiliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).
“Serikali kupitia MSD imeendelea kuwapa kipaumbele wazalishaji wa ndani kwa kuhakikisha malipo yanafanyika kwa wakati, jambo linalochochea uzalishaji na kuvutia uwekezaji zaidi,” alisema.
Aliongeza kuwa hatua hiyo imewezesha ongezeko la thamani ya ununuzi kutoka shilingi bilioni 15.9 mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni 98.72 mwaka 2024/2025.
Hata hivyo, alikiri kuwepo kwa changamoto kwa baadhi ya wazalishaji wanaoshindwa kufikia kiwango cha chini cha uzalishaji (minimum order quantity), hali inayosababisha baadhi ya bidhaa kununuliwa kupitia mawakala wao.
Pamoja na hayo, Mavere alisisitiza kuwa MSD itaendelea kuboresha mifumo yake ya ununuzi ili kuhakikisha upatikanaji wa dawa na bidhaa za afya unakuwa wa uhakika, endelevu na wenye kuzingatia thamani ya fedha za umma.





