Na Mwandishi Wetu,Kampala
Katika hatua inayoashiria kuimarika kwa nafasi ya Tanzania katika vita dhidi ya rushwa barani Afrika, Mtanzania Bi.Lilian William Kafiti amechaguliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Umoja wa Mamlaka za Kupambana Rushwa za Afrika Mashariki,(EAAACA) taasisi ambacho ni chombo muhimu katika kuratibu mapambano dhidi ya rushwa katika nchi za Afrika Mashariki.
Uamuzi huo ulipitishwa kwa kauli moja na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 16 wa taasisi hiyo uliofanyika Aprili 24, 2026, na kumfanya kuwa mmoja wa viongozi wachache wa Tanzania kushika nafasi ya juu katika taasisi za kikanda.
Kwa sasa Bi. Kafiti anahudumu kama Afisa Mchunguzi Mkuu katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ambako amejijengea sifa ya utendaji makini, weledi na uadilifu katika kushughulikia kesi nyeti za rushwa.
Ushindi wake haukuwa wa bahati nasibu, bali ulitokana na ushindani mkali uliowahusisha wagombea 89 kutoka nchi wanachama, wakiwemo Burundi, Djibouti, Ethiopia, Kenya, Rwanda, South Sudan, Uganda na Tanzania.
Uteuzi wake unakuja wakati ambapo EAAACA inaendelea kuimarisha jukumu lake la kuwa jukwaa la ushirikiano wa kikanda katika mapambano dhidi ya rushwa, uhalifu wa kifedha na ubadhirifu wa rasilimali za umma.
Taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2007 na makao yake makuu yako Kampala, Uganda, ambako sasa ndipo Bi. Kafiti atakapohamia kwa kipindi cha miaka sita kuhudumu katika wadhifa huo mpya.
Kutokana na uteuzi huo, atalazimika kuomba likizo kutoka serikalini ili kujiunga rasmi na Sekretarieti ya EAAACA, hatua inayodhihirisha uzito wa majukumu atakayobeba katika kusimamia operesheni za taasisi hiyo.
Hii ni nafasi inayohitaji uwezo mkubwa wa uongozi, uratibu wa sera na mikakati ya kikanda, pamoja na kuunganisha taasisi mbalimbali za kupambana na rushwa ili kufanya kazi kwa pamoja kwa ufanisi zaidi.
Majukumu ya EAAACA ni pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za kupambana na rushwa katika nchi wanachama, kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa muhimu za kiintelijensia, na kuratibu operesheni za pamoja zinazolenga kukabiliana na uhalifu wa kifedha unaovuka mipaka ya nchi.
Aidha, taasisi hiyo hutoa mafunzo, tafiti na msaada wa kitaalamu kwa taasisi wanachama ili kuongeza uwezo wao wa kuchunguza na kushughulikia vitendo vya rushwa kwa weledi wa hali ya juu.
Katika muktadha wa sasa wa utandawazi, rushwa imekuwa na sura mpya inayohusisha mitandao ya kimataifa ya fedha haramu, jambo linalohitaji ushirikiano wa karibu wa kikanda.
Kupitia EAAACA, nchi wanachama zimekuwa zikishirikiana katika kufuatilia fedha chafu, kurejesha mali zilizopatikana kwa njia haramu, na kuhakikisha wahusika wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Hivyo basi, nafasi ya Katibu Mtendaji ni kiini cha mafanikio ya taasisi hiyo.
Uchaguzi wa Bi. Kafiti unaipa Tanzania heshima kubwa katika jukwaa la kimataifa, huku ukionesha imani iliyopo juu ya uwezo wa wataalamu wake katika kusimamia masuala nyeti ya utawala bora.
Tanzania imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali ya kupambana na rushwa kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na taasisi nyingine za serikali, hatua ambazo zimeanza kuzaa matunda kwa kuimarisha uwajibikaji na nidhamu katika matumizi ya rasilimali za umma.
Kwa miaka ya hivi karibuni, juhudi za Tanzania zimejikita katika kuimarisha mifumo ya kisheria, kuongeza uwazi katika manunuzi ya umma, na kutumia teknolojia katika kufuatilia miamala ya kifedha.
Mafanikio haya yameifanya nchi kuonekana kama mfano wa kuigwa katika eneo la Afrika Mashariki, jambo lililochangia kwa kiasi kikubwa uteuzi wa Bi. Kafiti kushika nafasi hiyo ya juu.
Katika hotuba za kumuaga aliyekuwa Katibu Mtendaji aliyemaliza muda wake, viongozi wa EAAACA walisisitiza umuhimu wa kuendeleza mshikamano na kuongeza juhudi za pamoja ili kukabiliana na changamoto mpya za rushwa.
Waliweka bayana kuwa mafanikio yaliyopatikana hadi sasa yametokana na ushirikiano thabiti baina ya nchi wanachama na wadau wa maendeleo, na kwamba uongozi mpya unapaswa kuendeleza ari hiyo.
Kwa upande wake, matarajio ni makubwa kwa Bi. Kafiti kuleta mageuzi chanya yatakayosaidia kuimarisha zaidi taasisi hiyo na kuongeza ufanisi wake katika kutekeleza majukumu yake.
Uzoefu wake katika uchunguzi wa rushwa na uelewa wake wa mifumo ya kikanda vinatarajiwa kuwa chachu ya mafanikio mapya katika mapambano dhidi ya adui huyu wa maendeleo.
Kwa ujumla, uteuzi huu si tu mafanikio binafsi kwa Bi. Kafiti bali pia ni ushindi kwa Tanzania na ishara kuwa nchi inaendelea kusimama imara katika vita dhidi ya rushwa.
Ni hatua inayotuma ujumbe mzito kwamba Afrika Mashariki ina rasilimali watu wenye uwezo wa kuongoza mabadiliko na kujenga mustakabali wenye uwazi, uadilifu na uwajibikaji kwa vizazi vijavyo.




