PARIS, UFARANSA
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa, Mheshimiwa Saidi Othman Yakubu, leo amewasilisha rasmi nakala ya Hati zake za Utambulisho kwa Serikali ya Jamhuri ya Ufaransa, hatua muhimu inayomuwezesha kuanza kutekeleza majukumu yake ya kibalozi nchini humo.
Hafla hiyo ya kiitifaki imefanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Paris ambapo Balozi Yakubu alimpokea Balozi Mathieu Carmona, Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Itifaki katika Wizara ya Ulaya na Mambo ya Nje ya Ufaransa, aliyepokea nakala hizo kwa niaba ya Serikali ya Ufaransa.
Uwasilishaji wa nakala ya Hati za Utambulisho ni hatua ya awali ya kiitifaki inayomruhusu Balozi kuanza rasmi utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku, ikiwa ni pamoja na kusimamia shughuli za Ubalozi, kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, na kusukuma mbele ajenda za diplomasia ya uchumi kati ya Tanzania na Ufaransa.
Kwa mujibu wa taratibu za kidiplomasia za Jamhuri ya Ufaransa, Balozi Yakubu ataendelea na majukumu yake huku akisubiri kuwasilisha rasmi Hati za Utambulisho kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Ufaransa, Emmanuel Macron, tukio ambalo litakamilisha kikamilifu utambulisho wake kama Mwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini humo.
Katika mazungumzo yaliyofanyika baada ya uwasilishaji huo, pande zote mbili zilipata fursa ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu kuimarisha ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Ufaransa katika nyanja za kimkakati.





