Paris, Ufaransa – 25 Aprili 2026
Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa umeshiriki kikamilifu katika maonesho ya kitamaduni yaliyojulikana kama “Culture à l’Honneur l’Afrique”, yaliyofanyika katika Kituo cha Utamaduni na Kijamii cha Grésillons jijini Paris.
Katika maonesho hayo yaliyolenga kuadhimisha na kuenzi tamaduni za Bara la Afrika, banda la Tanzania limejitokeza kuwa moja ya vivutio vikuu, likivutia idadi kubwa ya washiriki na wageni waliopata fursa ya kujifunza kuhusu urithi wa kitamaduni wa Tanzania pamoja na vivutio vyake vya utalii.
Wageni waliotembelea banda la Tanzania walipata uzoefu wa kipekee kwa kuvalishwa mavazi ya asili ya Kimasai, hatua iliyoongeza mvuto na uhalisia wa utamaduni wa Kitanzania. Aidha, walipatiwa maelezo ya kina kuhusu vivutio maarufu vya utalii ikiwemo Hifadhi za Taifa, Mlima Kilimanjaro, Fukwe za Zanzibar pamoja na urithi wa kihistoria wa nchi.
Watumishi wa Ubalozi walitumia fursa hiyo kusambaza makabrasha mbalimbali ya utalii, kutoa maelezo ya kitaalamu kwa wageni pamoja na kuonesha makala na vielelezo vinavyoakisi uzuri na upekee wa Tanzania kama moja ya vivutio vinavyoongoza barani Afrika.
Katika kuonesha umuhimu wa soko la Ufaransa kwa sekta ya utalii, imeelezwa kuwa takriban watalii 120,000 kutoka Ufaransa hutembelea Tanzania kila mwaka, jambo linaloifanya Ufaransa kuwa moja ya masoko muhimu ya kimkakati katika juhudi za kukuza utalii wa Tanzania barani Ulaya.
Ushiriki wa Ubalozi katika maonesho hayo unaakisi dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuimarisha diplomasia ya utamaduni na uchumi, kwa kutumia majukwaa ya kimataifa kuitangaza Tanzania, kuvutia watalii na kuimarisha uhusiano wa watu kwa watu kati ya Tanzania na Ufaransa.
Maonesho hayo pia yalihusisha shughuli mbalimbali zikiwemo maonesho ya vyakula vya Kiafrika, muziki, ngoma za asili, pamoja na ubunifu wa sanaa, yakitoa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na kukuza uelewa wa tamaduni za Afrika katika jamii ya kimataifa.




