Na Mwandishi wetu, Monduli
MDAU wa maendeleo Taiko Kulunju amejitolea kutoa fedha za ujenzi wa uzio wa bweni la wasichana wanaosoma shule ya sekondari Moringe Sokoine iliyopo wilayani Monduli mkoani Arusha, waliokuwa wanakabiliwa na changamoto ya kukosa uzio kwenye bweni lao.
Mdau wa maendeleo Taiko akizungumza kwenye mahafali ya kidato cha sita ya shule hiyo amesema ataondoa changamoto hiyo ya uzito unaogharimu shilingi milioni 7 ili wasichana wanaosoma hapo walale kwa usalama bwenini na kuepusha wizi wa vitu vyao.
“Katika risala yenu changamoto ya ukosefu wa bweni la wasichana imenigusa, baada ya kutoa shilingi milioni nne nitamaliza iwe shilingi milioni saba maana nikianza kazi huwa napenda kumaliza,” amesema Taiko.
Amewaasa wahitimu wanaotarajia kufanya mtihani wao hivi karibuni kujipanga ipasavyo na kumtegemea Mungu ili waweze kufaulu.
“Elimu ndiyo jambo kubwa kwa sasa ninyi ni vijana tunatarajia mengi kwenu kwani hata serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inawajali vijana ndiyo sababu inatoa na mikopo kwao,” amesema Taiko.
Amesema kutokana na hali hiyo wazazi, walezi na jamii kwa ujumla inamatarajio makubwa kwao katika ufaulu mzuri pindi wakishamaliza kufanya mtihani wao.
Mkuu wa shule ya Moringe Sokoine, Lazaro Ndoki amemshukuru Taiko kwa kugharamia fedha za ujenzi wa uzio wa eneo la bweni la wasichana wa shule hiyo.
Ndoki amesema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1980 na aliyekuwa Waziri Mkuu hayati Sokoine ikiitwa Monduli sekondari ikilenga watoto wa jamii ya kifugaji wa wiilaya za Monduli, Simanjiro, Ngorongoro na Kiteto, wapate elimu.
“Baada ya kifo cha muasisi huyu mwaka 1984 jina la shule ilibadilishwa kwa heshima yake na kuitwa Moringe Sokoine kwa kumbukumbu ya heshima ya mwanzilishi huyu mwaka 1987,” amesema.
Amesema shule hiyo ina wanafunzi 335 wa kidato cha kwanza hadi cha sita, wakiwemo wahitimu 47 wa kidato cha sita, wavulana 26 na wasichana 21.
“Tuna imani na wahitimu hawa kufanya vyema kwani nyota njema huonekana asubuhi ila nawaasa huko duniani ni kugumu nina mnukuu mwanahabari prof Normn Cousin alisema msiba siyo kifo bali kinachoruhusu kifo wakati tungali hai,” amesema.
Mmoja kati ya wanafunzi wa kidato cha sita Enjo Silasi akisoma risala ameeleza kuwa ukosefu wa uzio kwenye bweni la wasichana ni changamoto kwao.




