Katibu Mkuu mpya wa jumuiya ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Patrick Mbundi amesema kuwa katika nafasi yake hiyo ataanza na vipaumbele muhimu ikiwemo kuimarisha soko la pamoja, kukuza biashara ya pamoja ndani nje ya nchi .
Ameyasema hayo jijini Arusha katika hafla ya makabithiano ya madaraka baina yake na Katibu mkuu aliyemaliza muda wake ,Veronica Nduva hafla iliyofanyika katika makao makuu wa jumuiya ya Afrika Mashariki.
Balozi Mbundi amesema kuwa atahakikisha kuna kuwepo usimamizi thabiti wa rasilimali, uwajibikaji na uwazi katika utekelezaji wa majukumu ya jumuiya kwa ujumla .
“ninachoomba kwa wanajumuiya wenzangu ni ushirikiano wa karibu ili niweze kufanikisha malengo yote niliyotapanga na kukabiliana na changamoto mbalimbali .”amesema Mbundi.
Makabidhiano hayo yamehitimisha rasmi kipindi cha uongozi wa Nduva, aliyeliongoza taasisi hiyo kwa msisitizo wa kuimarisha mshikamano wa nchi wanachama na kusukuma mbele ajenda za maendeleo ya kikanda, hususan katika nyanja za uchumi na ushirikiano wa kimkakati.
Balozi Mbundi amesema kuwa,katika kuhakikisha jumuiya inaendelea kuimarika ataendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa nchi wanachama na kuhakikisha biashara zinafanyika kwa umoja kwa nchi uanachama .
“Tutajenga barabara huku tukizingatia maswala ya mabadiliko ya tabia ya nchi na kuhakikisha tunaimarisha amani na usalama kwa nchi zote wanachama “.amesema Mbundi.
Akizungumza katika hafla hiyo ,Katibu mkuu aliyemaliza muda wake ,Veronica Nduva ameshukuru sana kwa namna ambavyo wana jumuiya walimwonyesha ushirikiano mkibwa kipindi cha uongozi wake huku akiwaahidi kuendelea kushirikiana katika kila jambo.
“Katika kipindi changu cha uongozi, hatua mbalimbali zimechukuliwa katika kuimarisha utekelezaji wa miradi ya pamoja, kukuza biashara ndani ya ukanda na kuweka mazingira rafiki ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo.”amesema Nduva.
Aidha, ameweka msisitizo mkubwa katika umuhimu wa kuendelezwa kwa mshikamano miongoni mwa nchi wanachama, akieleza kuwa mafanikio yaliyofikiwa yanahitaji kulindwa na kuendelezwa kupitia ushirikiano wa karibu wa wadau wote wa maendeleo ndani ya EAC.
Mabadiliko hayo ya uongozi yanakuja katika kipindi ambacho EAC inaendelea kupanuka na kuimarisha nafasi yake kikanda na kimataifa, hali inayoweka matarajio makubwa kwa uongozi mpya katika kusukuma mbele ajenda ya ujumuishaji wa kikanda na ustawi wa wananchi wake.





