Dar es Salaam
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imekagua utekelezaji wa ujenzi wa barabara za zenye urefu wa Kilomita 8.262 kwa kiwango cha lami zinazojengwa na TARURA kupitia mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II) katika Halmashauri ya Jiji la Ilala mkoani humo.
Akizungumza katika ziara hiyo leo Aprili 25, 2026, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Ado Shaibu amepongeza jitihada za serikali chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika. Pia amempongeza Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu kwa miongozo na usimamizi wa miradi hiyo katika Jimbo lake la Ilala.
”Kwa niaba ya wajumbe wa Kamati, tunatoa pongezi kwa Mhe. Waziri Prof. Shemdoe na Wizara nzima ya OWM- TAMISEMI, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Waheshimiwa Madiwani na viongozi wote wa mkoa kwa usimamizi wa miradi hii ambayo inakwenda kuleta tija kwa wananchi”, amesema.
Vilevile, Kamati imeipongeza TARURA kwa usimamizi wa miradi hiyo ambapo thamani ya fedha inaonekana na Kamati imewataka TARURA kuyafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa ikiwemo miradi kukamilika kwa wakati.
Aidha, Kamati imependekeza kuwepo na mpango wa pamoja wa Kitaifa wa mamlaka zenye miradi inayopita katika barabara kama sekta ya maji, umeme na simu kufanya kazi kwa pamoja na TARURA wakati wa utekelezaji wa miradi ya barabara ili kuiepushia hasara serikali.
”Mamlaka kama TANESCO, DAWASA na wengine ambao miradi yao inapita katika barabara, mamlaka hizi zikae pamoja na TARURA wakati wa usanifu wa miradi ya barabara ili kuepusha kubomoa na kujenga miradi iliyokamilika na inayofanya kazi ili kuipunguzia serikali gharama wakati wa utekelezaji wa miradi hii”, amesema.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI (Afya), Prof. Tumaini Nagu, kwa niaba ya Waziri wa OWM-TAMISEMI amewapongeza watumishi na wataalamu wa ofisi hiyo kwa moyo wa uzalendo na usimamizi mzuri wa miradi na kuwataka kuendelea kushirikiana kwa pamoja ili kuleta tabasamu kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, ameishukuru Kamati kwa ushauri wake wa kitaalamu na kwamba maagizo na maelekezo yote yaliyotolewa watasimamia, kufuatilia na kuzingatia pia amewashukuru Wabunge wote na wajumbe wa kamati kwa kupitisha bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa TARURA wilaya ya Ilala, Mhandisi John Chacha amesema ujenzi wa barabara za CBD Ilala ni mkopo nafuu toka Benki ya Dunia kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 23.5 ambapo mradi unatarajiwa kukamilika tarehe 14 Agosti, 2026.





