*Yasifiwa kwa mafanikio ya upandaji miti, yaungwa mkono vita ya tabianchi
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
DAR ES SALAAM: Magereza ya Ukonga yamepongezwa kwa mafanikio makubwa ya utunzaji wa mazingira baada ya kuonesha mfano bora wa upandaji na uhifadhi wa miti, hatua inayochangia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Pongezi hizo zimetolewa na Kamishna Mwandamizi wa Kikosi Maalum cha Magereza Tanzania jana Aprili 24,2026, Hamis Lissu, alipokutana na maafisa wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) waliotembelea magereza hayo kufanya tathmini ya miche iliyotolewa na wakala huo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Lissu alizitaka taasisi na wananchi kuongeza juhudi za upandaji miti na matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira na rasilimali za taifa.
Alisema utunzaji wa mazingira si jukumu la serikali pekee bali ni wajibu wa kila mmoja, akisisitiza kuwa hatua za sasa ndizo zitakazoamua mustakabali wa mazingira kwa vizazi vijavyo.
Kwa mujibu wa Lissu, miti iliyopandwa katika Magereza ya Ukonga imechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha hali ya hewa, kupunguza joto na kuongeza mvuto wa mazingira ya eneo hilo.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mwandamizi wa TFS, Happiness Kivuyo, alisema taasisi hiyo imeridhishwa na namna magereza hayo yalivyotunza miche waliyopewa.
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa TFS Kanda ya Mashariki, SACC Mathew Ntilicha, Kivuyo alisema miti mingi imekua vizuri na inaonesha usimamizi makini wa mazingira.
Alibainisha kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya TFS na taasisi za umma katika kusimamia rasilimali za misitu.
Aidha, aliwataka wadau wengine kuiga mfano huo kwa kuchukua miche kutoka TFS na kuipanda ili kuongeza uoto wa asili na kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Hatua ya Magereza ya Ukonga imeelezwa kuwa mfano bora wa kuigwa kitaifa, huku wataalamu wakisisitiza kuwa juhudi za pamoja ndizo zenye uwezo wa kuleta mabadiliko ya kudumu katika uhifadhi wa mazingira.





