Na OWM TAMISEMI, Longido-Arusha
Kilio cha muda mrefu cha wanafunzi wa Shule ya Sekondari Longido cha kutokuwa na bwalo la kisasa kimepata ufumbuzi baada ya Serikali kuahidi kutoa zaidi ya Shilingi Milioni 700 kwa ajili ya ujenzi wa bwalo jipya litakalokidhi mahitaji ya wanafunzi zaidi ya 3,000 wa shule hiyo.
Ahadi hiyo imetolewa leo Aprili 25, 2026 na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais -TAMISEMI anayeshughulikia Elimu,Mhe. Dkt Festo Dugange, wakati wa mahafali ya 21 ya kidato cha sita yaliyofanyika shuleni hapo wilayani Longido.
Dkt. Dugange ametoa ahadi hiyo baada ya kusikiliza risala ya wanafunzi wa kidato cha sita ambayo imeeleza changamoto iliyopo ya ufinyu bwalo , ikibainisha kuwa hali hiyo inatokana na idadi kubwa ya wanafunzi, hivyo kusababisha usumbufu wakati wa chakula na shughuli nyingine za kila siku.
Dkt. Dugange amesema Serikali imepokea kwa uzito mkubwa changamoto hiyo na imejipanga kuboresha mazingira ya wanafunzi.
“Serikali imewasikia. Tumejipanga kutoa zaidi ya Shilingi Milioni 700 kwa ajili ya ujenzi wa bwalo jipya litakalokidhi mahitaji ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Longido,” amefafanua.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mhe.Salumu Kalli, ameishukuru Serikali na kuwataka wahitimu hao kujiandaa vyema na mitihani yao ya taifa inayotarajiwa kuanza Mei 4, 2026, huku akisisitiza nidhamu na bidii kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Naye Mkuu wa Shule, Mwalimu Justine Swai, amesema walimu wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri kitaaluma kwakuwa wamewaandaa vyema na wana imani kuwa watafanya vizuri.





