Na.Sophia Kingimali.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema Nchi imejipanga vizuri kuhakikisha inalinda na kuendeleza vyanzo vya maji kwa maslahi ya wananchi.
Hayo ameyasema leo Aprili 24,2026 Jijini Dar es salaam kwenye kikao cha 13 cha Baraza la Mawaziri wa nchi wanachama wa Bonde la Mto Zambezi,ambapo ameeleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kulinda rasilimali za maji.
Aweso pia amewashukuru mawaziri kutoka nchi wanachama kwa ushirikiano wao, akibainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi nane zinazoshiriki kikamilifu katika juhudi za kuhifadhi na kusimamia rasilimali za bonde hilo.
Amesema kikao hicho cha mwaka huu kimefanyika nchini Tanzania ambayo imekuwa mwenyeji na mwenyekiti wa baraza hilo, huku akieleza kuwa muda wa uenyekiti wao umefikia ukingoni.
Kutokana na hilo, Aweso ametangaza kuwa Tanzania sasa inakabidhi rasmi nafasi ya uenyekiti kwa Zambia, huku akisisitiza kuwa bado nchi itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kulinda rasilimali za maji.
Ameongeza kuwa chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama kuhakikisha maji yanatunzwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Aweso amesisitiza kuwa rasilimali za maji ni msingi wa usalama wa taifa, akifafanua kuwa zinahitajika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji wa umeme na upatikanaji wa chakula cha kutosha.
Aidha, ameonya kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi, akitolea mfano hali ya mvua na mafuriko katika maeneo mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, hali inayohitaji hatua za pamoja.
Amesema katika kikao hicho, wajumbe watajadili utekelezaji wa mipango ya mwaka uliopita na kupitisha mipango mipya kwa mwaka ujao ili kuboresha usimamizi wa maji.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuanzisha miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa mabwawa ambayo yatasaidia kudhibiti mafuriko pamoja na kuimarisha kilimo na uzalishaji wa nishati.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji wa Zambia, Collins Zinzovu, amesema kikao hicho ni muhimu katika kufanya maamuzi yatakayosaidia kulinda rasilimali za maji zinazokabiliwa na changamoto nyingi.
Ameeleza kuwa ongezeko la watu, uchafuzi wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi vimeongeza shinikizo kwenye rasilimali hizo, hali inayohatarisha usalama wa chakula na maji.
Naye Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Mto Zambezi, Felix Ngamlagosi, amesema kikao hicho kinawakutanisha nchi nane wanachama kujadili utekelezaji wa mipango, kupitisha sera na kuimarisha ushirikiano kwa lengo la kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za maji.





