Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo na Mhadhiri wa UDOM, Dkt Alfred J. Meremo amesema hospitali hiyo imeendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na wanachuo, huku ikipanua wigo wa huduma muhimu zikiwemo za uchunguzi, matibabu na rufaa.
Dkt. Meremo ameeleza hayo kwa Wahariri wa vyombo vya habari mbalimbali waliotembelea katika hospitali hiyo wakiwa katika ziara ya Bohari ya Dawa MSD mkoani Dodoma
Amesema kwa sasa hospitali hiyo inatoa huduma mbalimbali ikiwemo (dialysis), huduma za kinywa na meno pamoja na huduma nyingine za kitabibu, huku jengo jipya la mionzi likiwa linaendelea kukamilishwa ili kuongeza ubora wa uchunguzi wa magonjwa.
Ameeleza kuwa katika jengo hilo jipya, hospitali inatarajia kuwa na vifaa vya kisasa kama CT Scan, Mammography na Fluoroscopy, huku huduma ya X-ray tayari ikiwa imeanza na kusaidia wagonjwa wengi.
Aidha, amesema mfumo wa mapokezi na huduma za dharura umeboreshwa, ambapo wagonjwa hupokelewa na kuhudumiwa kwa haraka kabla ya kupelekwa katika vitengo maalum kulingana na mahitaji yao ya kiafya.
Dkt Meremo ameongeza kuwa hospitali imeweka utaratibu wa kuhudumia makundi tofauti ikiwemo wanafunzi, watumishi na wananchi wa nje ili kupunguza msongamano na kuhakikisha huduma zinapatikana kwa wakati.
Amebainisha kuwa licha ya jitihada hizo, bado kuna changamoto ya upungufu wa watumishi wa afya, hali ambayo ni ya kitaifa kutokana na mahitaji makubwa ya huduma hizo.
Hata hivyo, amesema hospitali inaendelea kutumia wataalamu kutoka ndani ya chuo pamoja na wanafunzi wa fani za tiba na uuguzi kusaidia kupunguza pengo hilo na kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa bila kukwama.
Kwa upande wa dawa na vifaa tiba, amesema hospitali imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Bohari ya Dawa (MSD) ili kuhakikisha upatikanaji wake unakuwa wa uhakika na wa wakati.
Akizungumzia mafanikio ya kitaaluma, amesema UDOM imekuwa mstari wa mbele katika kuzalisha wataalamu wa afya, ikiwemo madaktari bingwa katika fani mbalimbali kila mwaka.
Kwa upande wake, Dkt Andrew Fanuel Lukwaro amesema hospitali hiyo inaendelea kutoa huduma za magonjwa ya figo ikiwemo upandikizaji, huku mahitaji ya huduma hizo yakiongezeka siku hadi siku.
Amesema changamoto kubwa ni gharama za matibabu pamoja na upatikanaji wa wafadhili wa viungo, akisisitiza umuhimu wa jamii kujitokeza kusaidia ndugu zao kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu.
Aidha, ameeleza kuwa wagonjwa wanaopandikizwa figo wanapaswa kufuata maelekezo ya kitabibu, hususan matumizi ya dawa maalum ili kuzuia mwili kukataa kiungo hicho.
Katika hatua nyingine, hospitali imeendelea kushirikiana na wadau wa kimataifa, wakiwemo wataalamu kutoka Japan, katika kuanzisha kituo cha umahiri cha upandikizaji wa figo na viungo vingine.
Akihitimisha, Dkt Sara Ludovic Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma amesema Hospitali ya hiyo imeboresha kwa kiwango kikubwa huduma za mama na mtoto, ikiwemo matibabu kwa watoto njiti na wanaohitaji uangalizi maalum, hatua iliyochangia kupunguza vifo vya watoto wachanga huku alipongeza serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Bohari ya Dawa MSD ambayo ndiyo inayowasambazia dawa na vifaa tiba. 





