Na Mwandishi wetu, Arumeru
MDAU wa madini ya Tanzanite, Hamisi Kim Komando ametoa zawadi ya kompyuta shule ya sekondari Makiba ya Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kwa ajili ya matumizi ya masomo ya Tehama.
Kim ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa bodi ya shule ya sekondari Makiba ameeleza hayo kwenye maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa shule hiyo mwaka 1996 na mahafali ya 15 ya kidato cha sita.
Amesema anaiunga mkono shule hiyo kwa kununua kompyuta moja kwa ajili ya wanafunzi hao waboreshewe suala zima la Tehama.
“Nawapongeza wanafunzi wote kwa kuhitimu kidato cha sita na ninawatakia kila la heri katika mtihani wenu mtakaofanya hivi karibuni,” amesema Kim.
Mkuu wa shule ya sekondari Makiba, Paul Kimaro amesema wameweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto ili wanafunzi wasome kidijitali kwa kutumia kompyuta.
Kimaro amesema wanaendelea kutafuta wadau wa maendeleo, kuboresha usimamizi wa rasilimali zilizopo na kuhamasisha matumizi sahihi ya Tehama katika elimu.
Amesema wanaendelea kutoa elimu ya maadili kwa wanafunzi ili waweze kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa kwa busara na nidhamu.




