Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Aprili 19, 2026
VIONGOZI mbalimbali wametakiwa kutendea haki nafasi walizonazo katika maeneo yao ya kazi ili kuleta matokeo chanya na kuacha alama, badala ya kufanya kazi kwa kupandisha mabega.
Rai hiyo imetolewa na aliyekuwa mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka, wakati akifunga mafunzo ya siku tano ya Uongozi Endelevu wa Usimamizi wa Mashirika ya Umma (SLIM PESA), yaliyofanyika kuanzia Aprili 13–18 katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kwamfipa Kibaha, yakihusisha washiriki 35 kutoka maeneo mbalimbali.
Vilevile, alisema katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, nchi inahitaji viongozi wenye uwezo wa kushindana kimataifa kwa ubunifu na weledi.
Mtaka aliwataka washiriki hao kujituma, kuwa na uadilifu na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuongeza tija katika maeneo yao ya kazi.
“Jiwekeni malengo makubwa; kupitia mafunzo haya, badilikeni kifikra na kiutendaji ili muwe chachu ya mabadiliko,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Profesa Marcellina Chijoriga, alisema washiriki wamepatiwa mafunzo katika maeneo mbalimbali ikiwemo uzalendo, usalama wa taifa, afya ya akili, itifaki na maadili, pamoja na mipango na usimamizi wa miradi ya maendeleo, uratibu na mawasiliano.
Aliwataka washiriki hao kuwa mabalozi wa mabadiliko kwa kutumia maarifa waliyoyapata katika kuboresha utendaji kazi kwenye taasisi zao.
Naye mshiriki wa mafunzo hayo, Jackie Ghikas, ambaye ni Mwanasheria Mwandamizi wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), aliahidi kuyatumia mafunzo hayo kwa vitendo ili kuleta mapinduzi ya maendeleo katika maeneo yao ya kazi.





