Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth), ambaye pia ni Rais wa zamani wa Jamhuri ya Malawi Mhe. Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 15 Aprili, 2026.
……………..
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amepokea ujumbe maalum kutoka kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Ayorkor Botchwey, uliowasilishwa na Mjumbe Maalum, Rais Mstaafu wa Malawi, Lazarus McCarthy Chakwera, katika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Ujumbe huo umebainisha maeneo ya kipaumbele yanayofuatiliwa na Jumuiya ya Madola, yakiwemo kuimarisha uwazi na ushirikiano katika tathmini ya matukio yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. Pia umeelekeza umuhimu wa kupanua ushiriki wa kisiasa, kuendeleza majadiliano ya vyama vya siasa na kuimarisha uwajibikaji wa taasisi za umma.
Katika maelezo yake, Katibu Mkuu Botchwey amesisitiza dhamira ya Jumuiya ya Madola kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha misingi ya demokrasia, utawala bora na maridhiano ya kitaifa kufuatia matukio ya uchaguzi huo. Ameeleza kuwa jumuiya hiyo iko tayari kusaidia juhudi za kujenga mazingira ya kisiasa yenye utulivu, ushirikishwaji mpana na kuaminiana kupitia mazungumzo na mageuzi ya taasisi.
Akizungumza wakati wa kupokea ujumbe huo, Rais Samia amesema Serikali inaendelea kushughulikia hali hiyo kupitia taasisi zake, akitaja hatua zilizochukuliwa ikiwemo kuundwa kwa Tume Huru ya Uchunguzi kwa lengo la kurejesha utulivu na kuimarisha uwajibikaji nchini. Ameongeza kuwa matokeo ya tume hiyo yataongoza hatua zinazofuata, zikiwemo uwajibikaji, maridhiano na mageuzi ya taasisi.
Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia mchakato wa maridhiano kwa kutumia majukwaa yaliyopo kisheria na kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa kisiasa na kijamii ili kuhakikisha amani na mshikamano vinaendelea kudumishwa nchini.
Kwa upande wake, Dkt. Chakwera amepongeza juhudi zinazofanywa na Tanzania na kueleza utayari wa Jumuiya ya Madola kuendelea kushirikiana na nchi katika kuimarisha utawala wa sheria, ushirikiano wa kisiasa na mshikamano wa kitaifa. Amesema ziara yake imelenga kufanya tathmini ya hali ya kisiasa na mchakato wa maridhiano, ambapo tayari amekutana na wadau mbalimbali wa kisiasa na kitaasisi nchini.
Dkt. Chakwera amehitimisha ziara yake ya kikazi nchini kama Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, akieleza matarajio ya kuona Tanzania ikiendelea kudumisha utulivu wa kisiasa na kuimarisha demokrasia kupitia mazungumzo na ushirikishwaji mpana wa wadau.





