Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam.
15/04/2025. Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kuzingatia usalama na afya mahali pa kazi ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Rai hiyo imetolewa leo na Meneja Rasilimali Watu wa JKCI Hospitali ya Dar Group Abdulrahman Muya wakati wa mafunzo yaliyotolewa na wataalamu kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) pamoja na wataalamu kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).
Muya alisema wafanyakazi wanapopata elimu kuhusu vihatahirishi vinavyoweza kujitokeza wakiwa mahali pa kazi inawasaidia kujilinda dhidi ya majeraha, mumivu ya viungo pamoja na kufahamu haki zao za fidia pindi wanapopatwa na ajali au madhara yanayotokana na kazi.
Kwa upande wake Afisa Utekelezaji kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Calvin Urassa alisema mfuko huo umeanzishwa na serikali kwa lengo la kushughulikia masuala ya fidia kwa mfanyakazi anayepata ajali kazini, kuugua au kufariki kutokana na kazi wanazozifanya.
Naye Mkaguzi Mazingira ya Kazi kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) Simon Lwaho alisisitiza juu ya umuhimu wa kuwepo kwa miundombinu bora na salama mahali pa kazi ili kuwawezesha wafanyakazi kutoa huduma kwa ufanisi na ustadi.
Wakizungumzia mafunzo hayo wafanyakazi wa JKCI wameshukuru kwa kupatiwa mafunzo ambayo yamewasaidia kuelewa kuhusu haki zao za msingi na kujua mbinu bora za kujilinda kiafya wanapokuwa mahali pa kazi.
“Mafunzo haya yamenisaidia kuelewa kwa kina ni aina gani ya mafao ninastahili na taratibu za kufuatwa iwapo nitapata ajali au madhara kazini”, alisema Daniel Mkuyu Afisa Uuguzi wa JKCI Dar Group.
“Nimejifunza kujali afya ya mwili niwapo kazini hususani kwa kuzingatia namna nzuri ya ukaaji ili kuepuka maumivu ya viungo”, alisema Afisa Muuguzi Salama Mohamed.




