NA DENIS MLOWE, IRINGA
WAKAZI wa maeneo yanayozunguka mgodi wa Lumwago, katika Mafinga Mjini mkoani Iringa, wameeleza malalamiko yao kuhusu ubovu wa miundombinu ya barabara, kukosekana kwa maji ya uhakika na kukatika mara kwa mara kwa umeme, wakisema kuwa changamoto hizo zimeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli zao za kila siku.
Wakizungumza katika mkutano wa Mbunge wa Mafinga Mjini, Dickson Lutevele, wananchi wamesema barabara nyingi zimeharibika kupita kiasi, hali inayosababisha adha kubwa kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri. Wameeleza kuwa safari za kutoka nyumbani kwenda sokoni zimekuwa za mateso kutokana na barabara kuteleza na mashimo makubwa, hali inayosababisha magari madogo na bajaji kupinduka. Baadhi ya wanawake, wakiwemo wajawazito na waliowahi kufanyiwa upasuaji, wameeleza kuwa hutumia nguvu nyingi kupita katika maeneo yenye miinuko na mashimo, jambo linaloweza kuhatarisha afya zao.
Pia, wakazi wa maeneo ya Boma hadi maeneo ya makaburini wametaja ubovu wa barabara kuwa kikwazo kikubwa licha ya kutumia vyombo vya usafiri vya kisasa. Wananchi wanaoishi maeneo ya Mkombwe na jirani na mgodi wa Lumwago wamesema changamoto hizo zimekuwa kero ya muda mrefu na zinahitaji ufumbuzi wa haraka.
Diwani wa Kata ya Boma, Baraka Kisakanike, amesema kuwa kata hiyo imekuwa ikikumbwa na tatizo la barabara hasa kipindi cha mvua kutokana na ukosefu wa mifereji imara ya kupitisha maji.
Amebainisha kuwa barabara kama ile ya Mbagala kuelekea Pareto zimekuwa hazipitiki kwa muda mrefu na ameiomba serikali kuingilia kati ili kutatua tatizo hilo.
Katika upande wa maji, wananchi wamelalamikia kukosekana kwa huduma hiyo licha ya kupata bili kila mwezi. Wamesema upatikanaji wa maji umekuwa wa kusuasua na kulazimisha baadhi ya familia kutumia muda mwingi kutafuta huduma hiyo muhimu.
Akijibu hoja hizo, Mbunge wa Mafinga Mjini, Dickson Lutevele, amesema serikali inaendelea kutekeleza mradi mkubwa wa maji unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 48, ambao utakapo kamilika utaongeza uzalishaji wa maji hadi lita milioni 11 kwa siku, wakati mahitaji ya Mafinga ni lita milioni 8 pekee.
Ameeleza kuwa mradi huo ambao umefikia asilimia 20.8 ya utekelezaji ni miongoni mwa miradi ambayo iko katika miji 28 inayoendelea nchini.
Aidha, amesema mradi huo unaoendelea katika jimbo hilo utazalisha lita milioni 11 za maji kwa siku, na endapo kila mwananchi atapata maji Mafinga tutakuwa na akiba ya maji lita milioni 4 kwa siku hatua itakayosaidia kupunguza tatizo la upungufu wa maji.
Kuhusu barabara, mbunge Lutevele amesema kuwa wataendelea kushirikiana na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha barabara korofi zinakarabatiwa pindi mvua zitakapopungua.
Wananchi wa Mafinga Mjini wameiomba serikali kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo ili kuboresha huduma za kijamii, ambazo wanasema zimekuwa zikikwamisha shughuli za kiuchumi na maendeleo katika maeneo yao.




