NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Mafinga Mjini, Mheshimiwa Dickson Lutevele Villa, ametimiza ahadi yake kwa kukabidhi jumla ya meza 90 kwa wajasiriamali wa Soko la Mashujaa, ikiwa ni jitihada za kuwawezesha kufanya biashara katika mazingira tulivu na yenye mpangilio.
Akizungumza na wananchi na wajasiriamali wa soko hilo katika Halmashauri ya Mji Mafinga, Mheshimiwa Villa alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya dhamira yake ya “kuwatua sinia kichwani” akinamama na vijana wanaofanya biashara ndogondogo, ili waweze kupata eneo maalumu la kufanyia shughuli zao kwa utulivu.
Mheshimiwa Villa alisisitiza kuwa ameamua kugawana na wananchi kile kidogo alichonacho ili kuupa heshima mtaji wa wajasiriamali wadogo ambao wengi wao huanza biashara kwa mitaji midogo.
Aliongeza kuwa kukosekana kwa vifaa kama meza kumekuwa kikwazo kwa baadhi ya wajasiriamali kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.
Aidha, alitoa wito kwa Halmashauri ya Mji Mafinga kuhakikisha maeneo rasmi ya kufanyia biashara yanaandaliwa, ili kutoa nafasi kwa wafanyabiashara hao kuuza bidhaa zao katika sehemu salama na zenye muonekano mzuri kwa wateja.
Diwani wa Kata ya Boma, Mheshimiwa Baraka Kisakanike, aliwataka wajasiriamali waliopokea meza hizo kufuata utaratibu wa serikali kwa kufanya biashara katika maeneo yaliyopangwa na kuepuka kujiwekea maeneo kiholela.
Awali, Mwenyekiti wa Soko la Mashujaa, Bw. Devick Kihindo, alimwomba Mbunge kuwatafutia eneo jipya na pana zaidi kwa ajili ya biashara, kutokana na idadi kubwa ya wajasiriamali wanaohitaji nafasi ya kufanyia shughuli zao.
Baadhi ya wajasiriamali waliopokea meza hizo walimshukuru Mbunge kwa msaada huo na kuahidi kufanya kazi kwa nidhamu katika maeneo ambayo watapangiwa na serikali.
