Na Silivia Amandius
Bukoba.
Mafunzo ya usuluhishi wa ndoa yanayoendeshwa na Wizara ya Katiba na Sheria yameendelea kuleta mwanga mpya katika jamii, huku yakitajwa kuwa nyenzo muhimu ya kupunguza migogoro ya kifamilia na kuimarisha mshikamano wa jamii.
Mafunzo hayo yalioendelea Kwa siku ya pili katika ukumbi wa mkuu wa mkoa wa kagera yamewakutanisha wajumbe wa mabaraza ya kata pamoja na wataalamu mbalimbali ili kuwajengea uwezo wa kushughulikia changamoto za ndoa kwa ufanisi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ndg. John Bundala alisisitiza umuhimu wa mabaraza ya usuluhishi wa ndoa kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya haki, maadili na usawa. Alieleza kuwa mabaraza hayo hayana jukumu la kutoa hukumu, bali kusaidia wanandoa kufikia muafaka kupitia mazungumzo na ushauri wa kitaalamu.
Kwa upande wa washiriki, mmoja wa wajumbe, Mwinyi Mohamed Mwinyi, alisema kuwa mafunzo hayo yamewapa uelewa mpana juu ya namna bora ya kushughulikia migogoro ya wanandoa, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo baadhi ya migogoro ilichukuliwa kuwa ni jambo la kawaida. “Tumegundua kuwa migogoro ya ndoa ina athari kubwa si tu kwa wanandoa, bali pia kwa watoto na jamii kwa ujumla,” alieleza.
Naye Idrisa Murashan Muzo alibainisha kuwa ukosefu wa elimu kuhusu usuluhishi wa ndoa umekuwa chanzo cha ongezeko la migogoro na talaka zisizo za lazima. Aliongeza kuwa kupitia mafunzo hayo, wamejifunza mbinu za mazungumzo, ushauri na namna ya kuwasaidia wanandoa kurejesha maelewano bila kuvunja ndoa zao.
Wataalamu waliotoa mafunzo hayo walieleza kuwa ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali za serikali ni muhimu katika kuhakikisha migogoro ya ndoa inatatuliwa kwa ufanisi. Walitaja ofisi za watendaji wa kata, wenyeviti wa mitaa na vitongoji, pamoja na maafisa ustawi wa jamii na dawati la jinsia kuwa nguzo muhimu katika kutoa msaada wa awali kwa wanandoa wenye migogoro.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, ofisi za ustawi wa jamii na dawati la jinsia hutoa ushauri nasaha na msaada wa kisaikolojia kwa wanandoa kabla ya kuwapeleka kwenye mabaraza ya usuluhishi ikiwa hali itahitaji hatua zaidi. Mfumo huu unalenga kuhakikisha kuwa migogoro inatatuliwa kwa njia ya amani na kulinda ustawi wa familia.
Washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuwa ujuzi walioupata utasaidia kuimarisha utendaji wa mabaraza ya usuluhishi wa ndoa, hasa ikizingatiwa kuwa wajumbe hubadilika mara kwa mara. Wameongeza kuwa mafunzo ya mara kwa mara ni muhimu ili kuhakikisha viongozi hao wanakuwa na mbinu bora za kisasa za kushughulikia migogoro.
Kwa ujumla, mafunzo haya yameonekana kuwa chachu ya kujenga familia imara, kupunguza migogoro ya ndoa na kusaidia malezi bora ya watoto, hatua inayochangia kujenga jamii yenye maelewano na taifa lenye ustawi endelevu.





