Na OWM – TAMISEMI, Bumbuli
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM -TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema kuwa amezindua madarasa matatu katika Shule ya Sekondari Kilivicha wilayani Bumbuli ambayo yataondoa changamoto ya msongamano wa wanafunzi madarasani, uliokuwa ukiikabili shule hiyo kwa muda mrefu.
Prof. Shemdoe ameongeza kuwa madarasa hayo pia ni sehemu ya maandalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka 2028 ambao watakuwa wamehitimu darasa ya sita na la saba kwa pamoja na kutakiwa kujiunga na kidato cha kwanza kutokana na mabadaliko ya mtaala mpya wa elimu unaotekelezwa na Serikali.
Prof. Shemdoe amesema hayo leo Machi 21, 2026 wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa madarasa hayo matatu yaliyojengwa kwa ufadhiri wa taasisi ya VUGA DELOPMENT INITIATIVE kwa gharama ya Shilingi Milioni 84,086,600/=.
“Ni ukweli usiopingika kwamba, ujenzi wa madarasa haya utaondoa msongamano wa wanafunzi madarasani na ni maandalizi ya kupokea wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2028, mara baada ya kumaliza darasa la sita na la saba kwa pamoja kwa mujibu wa mtaala mpya wa elimu,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe amemshukuru Bw. Rama Kaoneka ambaye ni Meneja wa Miradi wa Taasisi ya A BETTER WORLD CANADA ambaye pia ni kiongozi wa Taasisi ya VUGA DEVELOPMENT INNITIATIVE ambazo zimeshirikiana kufadhili ujenzi wa madarasa hayo matatu katika shule hiyo ya Sekondari Kilivicha.
Akizungumzia jitihada za Serikali za kuboresha miundombinu ya Elimu, Prof. Shemdoe amesema, Serikali inayongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mwaka huu wa fedha imeleta Bumbuli Shilingi Bilioni 3.2 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Shule za Msingi na Shilingi Bilioni 2.1 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Shule za Sekondari.
Aidha, Prof. Shemdoe amemuelekeza Katibu Mkuu wa Ofisi yake kuhakikisha anatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya fizikia na biolojia katika Shule ya Sekondari Kilivicha kwenye Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/27 ambayo maandalizi yake yanaendelea.
Kwa upande wake Bw. Kaoneka amesema kuwa, wamefadhili ujenzi wa madarasa hayo ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na ufundishaji shuleni hapo.
Mwanafunzi wa shule hiyo Bw. Emmanuel Francis Michael amesema kwamba miundombinu hiyo ya madarasa iliyojengwa itamuwezesha kufikia ndoto yake ya kuwa rubani, na kuongeza kuwa jamii itegemee ufaulu mzuri kutoka kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kilivicha.
Naye, Mkazi wa Kijiji cha Kivilicha Bw. Moses Thomas amemshukuru Prof. Shemdoe kwa kuzindua madarasa hayo matatu ambayo yatawawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora, na kuongeza kuwa madarasa hayo yataleta tabasamu kwa wanafunzi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kilivicha Bi. Sophia Dossa ameshukuru kwa kujengewa madarasa mapya na kuahidi kwamba madarasa hayo yatainua kiwango cha taaluma katika shule hiyo ya Sekondari ya Kilivicha.





