Waziri wa Nchi wa Ireland, Mhe. E. Christopher O’Sullivan, akiongozana na Balozi wa Ireland nchini, Nicola Brennan, wamefanya ziara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa lengo la kujionea huduma za matibabu ya saratani kwa watoto zinazofadhiliwa na Serikali ya nchi hiyo kupitia Taasisi ya Tumaini La Maisha.
Ziara hiyo pia imelenga kuonesha programu jumuishi za huduma, matibabu na msaada kwa watoto wenye saratani nchini Tanzania, zinazowawezesha kupata matibabu bora yanayookoa maisha .
Akizungumza wakati wa ziara hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Dkt. Faraja Chiwanga, ameeleza kuwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Serikali ya Ireland na taasisi mbalimbali umechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za matibabu ya saratani kwa watoto na kuongeza matumaini ya kupona kwa watoto wanaopatiwa huduma hizo.





