Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akimpokea mtoto Grace Samia Suluhu kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Tukai, tarehe 11 Machi, 2026 Ikulu Chamwino, Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na mtoto Grace Samia Suluhu aliyemuasili tarehe 11 Machi, 2026, Ikulu Chamwino, Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea cheti cha kuzaliwa cha mtoto Grace Samia Suluhu kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Tukai, Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma, tarehe 11 Machi, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Tukai, Afisa Muuguzi Msaidizi II Hospitali ya Mji Nzega Bi. Mariam Amasha Usangira, Bi Lucia Philipo Saitoti pamoja na Tatu Abdi Baraka (aliyembeba mtoto Grace Samia Suluhu), Ikulu Chamwino, Dodoma, tarehe 11 Machi, 2026.
………….
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemuasili mtoto mchanga wa kike leo tarehe 11 Machi, 2026, katika makazi yake, Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma.
Mtoto huyo aliyepewa jina la Grace Samia Suluhu Hassan alitelekezwa mjini Nzega, mkoani Tabora, na amekabidhiwa kwa Rais Dkt. Samia na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Tukai.
Akizungumza wakati wa kumkabidhi mtoto huyo, Mkuu wa Wilaya Tukai alisema mtoto huyo aliokotwa tarehe 17 Januari, 2026 akiwa ametelekezwa katika eneo jirani na nyumba ya wageni ya Kasulu, Nzega Mjini.
Alieleza kuwa baada ya kupokea taarifa hizo, alishirikiana na Jeshi la Polisi kumchukua mtoto huyo na kumpeleka hospitalini kwa uchunguzi na uangalizi, huku juhudi za kumtafuta mama yake zikiendelea bila mafanikio.
Rais Dkt. Samia amemkaribisha mtoto huyo katika familia yake na kuahidi kumpatia malezi, ulinzi na huduma zote muhimu ili akue katika mazingira salama na yenye upendo.
“Wanaotupa watoto hawajui wanalolifanya. Kuliko kumtupa mtoto ni afadhali ukamkabidhi katika mamlaka za kisheria au kituo cha kulelea watoto. Kila mtoto aliyezaliwa ni hazina, na hatuijui kesho yake,” alisema Rais Dkt. Samia.



