Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati inayolenga kuimarisha sekta ya mafuta na gesi asilia nchini, kuongeza upatikanaji wa nishati pamoja na kufungua fursa za ajira kwa vijana.
Akizungumza na waandishi wa habari Machi 11,2026 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC,Bw. Mussa Mohammed Makame, amesema kuwa miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa miongoni mwa miradi hiyo ni Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ambapo TPDC ina umiliki wa asilimia 15. Amesema kuwa mradi huo umefikia takribani asilimia 81 ya utekelezaji na unahusisha ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Aidha amebainisha kuwa kupitia mradi huo Watanzania wananufaika na ajira, fursa za zabuni na kandarasi pamoja na uhamishaji wa teknolojia na ujuzi, huku ujenzi wake ukitarajiwa kukamilika ifikapo Julai mwaka 2026.
Makame amesema kuwa Serikali pia ipo katika hatua za mwisho za majadiliano ya utekelezaji wa Mradi wa uchakataji na usindikaji wa gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) unaotarajiwa kugharimu takribani dola za Marekani bilioni 42.
Amesema kuwa mradi huo ni uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati na unatarajiwa kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha biashara ya gesi katika ukanda na kimataifa.
Aidha amebainisha kuwa TPDC tayari imeanza maandalizi ya kitaasisi na kiufundi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ikiwa ni pamoja na kuimarisha rasilimali watu, mifumo na usimamizi wa miundombinu.
Makame ameongeza kuwa Shirika pia linaendelea na mradi wa uchorongaji wa visima vitatu vipya vya gesi asilia katika eneo la Mnazi Bay mkoani Mtwara unaolenga kuongeza uzalishaji wa gesi asilia nchini.
Amesema kuwa uchorongaji wa kisima cha kwanza ulianza Februari 6, 2026 na hadi sasa utekelezaji umefikia asilimia 27 huku mradi huo ukitarajiwa kuongeza uzalishaji wa gesi kwa takribani futi za ujazo milioni 45 kwa siku.
Aidha amebainisha kuwa TPDC inaendelea kutekeleza mradi wa uchorongaji wa visima katika kitalu cha Ruvuma (Ntorya) pamoja na ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Ntorya kwenda kiwanda cha kuchakata gesi Madimba mkoani Mtwara.
Amesema kuwa mradi huo utasaidia kuongeza uzalishaji wa gesi asilia kwa takribani futi za ujazo milioni 60 na utaimarisha usalama wa nishati nchini.
Makame amesema kuwa Shirika pia linaendelea na mradi wa uchukuaji wa taarifa za mitetemo ya mfumo wa 3D katika kitalu cha Lindi-Mtwara kwa lengo la kubaini maeneo yenye uwezekano wa kuwa na mafuta au gesi asilia.
Aidha amebainisha kuwa mradi huo unatarajiwa kugharimu takribani shilingi bilioni 107 na utasaidia kuongeza uwezekano wa ugunduzi mpya wa rasilimali za gesi nchini.
Amesema kuwa TPDC pia linaendelea na mradi wa utafutaji wa mafuta katika kitalu cha Eyasi Wembere kinachopatikana katika mikoa ya Singida, Tabora, Simiyu, Arusha na Shinyanga.
Amesema kuwa hadi sasa Shirika linaendelea na uchukuaji wa taarifa za mitetemo za mfumo wa 2D na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2027.
Makame ameongeza kuwa TPDC inaendelea kupanua miradi ya usambazaji wa gesi asilia kwa matumizi ya viwandani, majumbani na kwenye vyombo vya usafiri katika mikoa mbalimbali nchini.
Amesema kuwa hadi sasa jumla ya vituo 14 vya kujaza gesi asilia kwenye magari (CNG) vimekamilika na vinaendelea kutoa huduma kwa vyombo mbalimbali vya usafiri.
Aidha amebainisha kuwa matumizi ya gesi asilia kwenye sekta ya usafirishaji yatasaidia kupunguza utegemezi wa mafuta kutoka nje ya nchi pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa vyombo vya moto.
Makame amesema kuwa upanuzi wa matumizi ya gesi asilia majumbani ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia, ambapo hadi sasa nyumba zaidi ya 2,500 zimeunganishwa na mtandao wa mabomba ya gesi asilia.
Ameongeza kuwa miradi hiyo pia inaendelea kufungua fursa mbalimbali za ajira, mafunzo na ushiriki wa vijana katika sekta ya nishati huku akibainisha kuwa takribani asilimia 79 ya wafanyakazi wa TPDC ni vijana.
Aidha amebainisha kuwa kupitia utekelezaji wa miradi hiyo, vijana wanapata fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, mafunzo ya vitendo pamoja na ushiriki katika zabuni za huduma mbalimbali zinazohusiana na sekta ya mafuta na gesi nchini.
Akizungumzia Hali ya upatikanaji wa mafuta nchi, Bw. Makame , amesema kuwa mafuta ya petroli na dizeli yanapatikana nchini kwa wingi na hakuna changamoto yoyote inayotarajiwa kuwaathiri wananchi, hata katika kipindi hiki ambacho dunia inashuhudia mvutano wa vita katika eneo la Mashariki ya Kati.
Ameongeza kuwa kwa sasa changamoto ndogo inayoweza kujitokeza ni ongezeko la bei ya mafuta kutokana na mabadiliko ya soko la kimataifa, hata hivyo serikali kupitia Wizara ya Nishati tayari imeweka mipango ya dharura ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kwa wananchi.



