Na. Sophia Kingimali, Dar es Salaam
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imeendelea kutoa elimu kwa viongozi wa vyama vya siasa kuhusu umuhimu wa kuwasilisha taarifa za gharama za uchaguzi kwa wakati, hatua inayolenga kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa kidemokrasia nchini.
Akizungumza leo Machi 10, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo ya namna ya kujaza fomu za gharama za uchaguzi, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohamed Ally Ahmed amesema sheria ya gharama za uchaguzi inavitaka vyama na wagombea kuwasilisha taarifa zinazoonyesha vyanzo na matumizi ya fedha zilizotumika katika kampeni.
Amesema utekelezaji wa sheria hiyo unasaidia kuhakikisha fedha zinazotumika katika siasa zinatoka katika vyanzo halali na kuzuia matumizi ya fedha chafu au ushawishi kutoka nje ya nchi ambao unaweza kuathiri misingi ya demokrasia.
Ahmed pia amevishukuru vyama vya siasa kwa ushirikiano waliouonesha wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita wa Oktoba 29, akibainisha kuwa vyama vingi vilishiriki katika uchaguzi huo kwa kuzingatia misingi ya katiba na sheria za nchi.
Ameeleza kuwa kuwepo kwa ukomo wa matumizi ya fedha katika kampeni kunasaidia kuweka usawa kati ya vyama vikubwa na vidogo, hivyo kutoa nafasi sawa ya ushindani katika uchaguzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatibu amesema ni muhimu kwa viongozi wa vyama kujaza kwa usahihi fomu za taarifa za gharama za uchaguzi ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za kisiasa.
Amesema mafunzo yanayotolewa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa yanawalenga makatibu wakuu wa vyama, wasimamizi wa uchaguzi pamoja na wadhamini ili kuwajengea uwezo wa kuelewa na kutekeleza ipasavyo matakwa ya sheria.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Esther Thomas amesema sheria ya gharama za uchaguzi imekuja wakati muafaka kwani inasaidia kudhibiti matumizi makubwa ya fedha katika kampeni na kuzuia vitendo vya rushwa kwa wapiga kura.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo ameipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kuandaa warsha hiyo, akisema imeongeza uelewa kwa vyama kuhusu wajibu wao wa kuwasilisha taarifa za matumizi na vyanzo vya fedha zilizotumika katika uchaguzi.




