……
Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
Waziri wa Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ni nguzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo na kukuza uchumi wa taifa.
Hayo ameyasema leo Mach 9,2026 Jijini Dar es salaam wakati akifungua kongamano la kujadili nafasi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) lililoandaliwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), amesema serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki ili sekta binafsi iweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Amesema Tanzania imejiwekea malengo makubwa ya kukuza uchumi katika miaka 25 ijayo kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kuongeza ukubwa wa uchumi hadi kufikia zaidi ya dola trilioni moja za Marekani.
“Kufikia malengo hayo tunahitaji mabadiliko ya kimfumo na ushiriki mkubwa wa sekta binafsi,kwani serikali haiwezi kufanya kila kitu peke yake katika shughuli za kiuchumi”,Amesema Profesa Kitila.
Aidha ameeleza kuwa jukumu la serikali ni kuweka sera, sheria na usimamizi wa jumla wa uchumi, huku shughuli nyingi za kiuchumi zikitekelezwa na sekta binafsi ili kuongeza ufanisi na kuharakisha maendeleo.
Ameongeza kuwa katika mpango wa nne wa maendeleo wa miaka mitano unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka 2026/2027, serikali imeweka malengo kadhaa ikiwamo kuimarisha uthabiti wa uchumi, kuboresha miundombinu ya usafiri na kuongeza tija katika sekta za uzalishaji.
Aidha amesema mpango huo unahitaji takribani Sh trilioni 477 kwa ajili ya utekelezaji wake, ambapo zaidi ya asilimia 70 ya fedha hizo zinatarajiwa kutoka katika sekta binafsi kupitia uwekezaji na mifumo mbalimbali ya ubia.
Profesa Mkumbo amesema hadi sasa Tanzania imeanza kutekeleza miradi kadhaa kupitia mfumo wa PPP katika sekta mbalimbali ikiwamo usafiri, miundombinu na huduma za biashara, huku mingine ikiwa katika hatua mbalimbali za maandalizi.
Hata hivyo Profesa Kitila amekiri kuwa kasi ya utekelezaji wa miradi ya PPP bado ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya miradi iliyopangwa, jambo linaloifanya serikali kuendelea kuboresha mifumo ya kisheria na kiutendaji ili kuongeza ufanisi.
Amesema serikali pia inaendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na kuhamasisha taasisi za umma kutumia mfumo wa PPP pale ambapo miradi inaweza kutekelezwa kwa ufanisi zaidi na sekta binafsi.
Profesa Mkumbo amehitimisha kwa kueleza kuwa kongamano hilo ni jukwaa muhimu la wadau kubadilishana mawazo na kutoa ushauri kwa serikali kuhusu namna bora ya kutumia ubia wa sekta ya umma na binafsi ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), David Kafulila amesema jukumu kuu la taasisi hiyo ni kuratibu ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inayoweza kufanywa na sekta binafsi inatekelezwa kwa ufanisi na kuisaidia serikali kupunguza mzigo wa kifedha.
Kafulila amesema kongamano hilo ni mwanzo wa majadiliano ya mara kwa mara yatakayokuwa yakifanyika kila mwezi kwa lengo la kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwamo wanazuoni, wataalamu wa uchumi, sekta binafsi na taasisi za serikali ili kujadili masuala ya maendeleo ya uchumi na utekelezaji wa miradi ya ubia.
Ameongeza kuwa majadiliano hayo yatasaidia kutoa mawazo na ushauri kwa serikali kuhusu namna bora ya kutumia ubia wa sekta ya umma na sekta binafsi, huku yakitoa fursa kwa wadau kuuliza maswali, kutoa mapendekezo na kushiriki katika kujenga uchumi imara wa taifa.




