Na Mwandishi Wetu,Mbinga
WANAWAKE wajasiriamali wa wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma,wametakiwa kuwa waaminifu kwa kurudisha mikopo ya asilimia 10 kwa wakati inayotolewa na Halmashauri za wilaya ili kutoa fursa kwa wanawake wengine waweze kukopa kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za maendeleo.
Wito huo umetolewa jana na Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Ruvuma Mheshimiwa Happy Ngwando,wakati akizungumza na wanawake na viongozi wa wilaya ya Mbinga kwenye sherehe ya siku ya wanawake Duniani wilaya ya Mbinga iliyofanyika katika ukumbi wa One Pasific Mbinga mjini.
Ngwando alisema,fedha zinazotolewa na Serikali kupitia Halmashauri za wilaya kwa ajili ya kukopesha makundi maalum ya wanawake,vijana na walemavu siyo sadaka ni lazima zirejeshwe ili kutoa nafasi kwa watu wengine waweze kukopa na kuanzisha miradi ambayo itawezesha kujiinua kiuchumi na kuondokana na umaskini.
Ngwando,amewahimiza wanawake wa Mkoa wa Ruvuma,kuanzisha miradi mbalimbali ambayo itawaingizia kipato ili kuwa na nguvu ya kiuchumi na kuchangia matumizi kwenye kwenye familia zao badala ya kuwategemea wanaume kwani hatua hiyo itawasaidia kuheshimika.
“Uchumi hauleti mapenzi,lakini hustawisha sana mapenzi,mwanamke ukipata fedha kwenye vikoba au kutoka kwenye yoyote ilie hakikisha sehemu ya fedha hizo zinatumika kwenye matumizi ya familia,lakini msisahau suala la heshima hata kama mume hana fedha”alisema
Aidha,amewataka kutumia taasisi za fedha zinazotambulika kisheria kama vile benki kwenda kukopa ili kuendeleza shughuli zao na kuepuka mikopo ya kausha damu ambayo imekuwa chanzo cha umaskini na fedhea kubwa kwa baadhi ya familia hapa nchini.
Katika hatua nyingine Ngwando,amewakumbusha wanawake kuwa karibu na Mungu kwa kufanya ibada wakati wote ili kujenga familia yenye maadili mema ambayo haitajiiingiza kwenye matendo mabaya yakiwemo ukatili wa kijinsia,wizi na ulevi kupindukia.
“Miaka ya nyuma sisi tukiwa wadogo mtoto hasiyetaka kwenda kanisani hapewi chakula,nawaomba sana mama zangu na wanawake wote kwa ujumla tusikubali kuwaacha watoto nyumbani bila kwenye kanisani au misikitini,hii itatusaidia sana kuwa na kizazi bora na mtoto anayemcha Mungu na kutenda matendo mema ni rahisi kufanikiwa katika maisha yake”alisema.
Amewaasa wanawake hao,kuwa na upendo kwa watoto na kujiepusha na vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa chanzo cha watoto kukimbia nyumbani na hata wanapokuwa watu wazima ni rahisi kulipiza vile walivyofanyiwa na wazazi kwa watoto wao.
Mwalimu wa chuo cha maendeleo ya jamii(FDC)wilaya ya Mbinga Regina Komba,amewataka wazazi kuhakikisha wanapeleka watoto wao shule ili kuwajengea msingi wa kwanza kimaisha na kuwaeleza watoto ukweli kwamba hakuna maisha rahisi bila kufanya kazi.
Mwenyekiti wa kikundi cha Wapambanaji Group Winfrida Mbulingwe,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya makundi ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu ambayo yamesaidia kujikwamua kiuchumi.




