Akizungumza wakati wa kutoa taarifa hiyo, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Iringa, Victor Swella alisema kuwa dhamira ya taasisi hiyo kuendelea kulinda maslahi ya wananchi ambapo katika kipindi hicho, TAKUKURU kwa ushirikiano na TANROADS ilibaini mianya ya upotevu wa mapato katika maeneo ya hifadhi za barabara, ambapo baadhi ya watu binafsi walikuwa wakinufaika isivyo halali.
Alisema kuwa Kupitia uchunguzi uliofanyika katika maeneo ya Ndiuka, Ifunda, Ilula Mtua na Ruaha Mbuyuni, kiasi cha Shilingi 106,192,180 kilirejeshwa na sasa kimeingizwa kwenye mfumo wa kidigitali wa ukusanyaji chini ya TANROADS.
Katika jukumu lake la kuzuia rushwa, TAKUKURU ilifanya uchambuzi wa mifumo ya uendeshaji wa vyombo vya watumia maji katika Wilaya ya Iringa kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha mifumo ya serikali.
Swella alisema kuwa Taasisi hiyo iliielekeza RUWASA kuharakisha ufungaji wa dira za maji kwa wateja wote, sambamba na kutekeleza miongozo ya serikali. TAKUKURU imeahidi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa agizo hilo.
TAKUKURU Iringa iliendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi ya elimu kupitia mpango wa BOOST katika shule 47 za msingi zenye thamani ya Shilingi 7,517,265,452. Baada ya kubaini baadhi ya miradi kutokuwa na vitabu muhimu vya kumbukumbu kama store ledger, receipt vouchers na issue vouchers, taasisi hiyo ilitoa elimu kwa kamati za ujenzi, na hatimaye vitabu hivyo viliwasilishwa na kuanza kutumika rasmi.
Katika kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu madhara ya rushwa, TAKUKURU iliwafikia wananchi 5,697 kupitia mbinu mbalimbali ikiwemo mikutano ya hadhara, onesho la uhamasishaji, uimarishaji wa klabu za wapinga rushwa, vipindi vya redio na semina za elimu kwa umma.
Amesema Uhamasishaji huu umeongeza uelewa wa wananchi na kubadili mitazamo katika kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha Oktoba–Desemba 2025, malalamiko 29 ya vitendo vya rushwa yalipokelewa. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni kesi mbili kuendelea kusikilizwa mahakamani, kesi moja mpya kufunguliwa na kesi moja Serikali kushinda.
Kwa kipindi cha Januari–Machi 2026, TAKUKURU Iringa imepanga kuendelea kuimarisha uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za umma kupitia mikakati mbalimbali, ikiwemo kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya elimu, afya, miundombinu na umwagiliaji; kufanya tathmini ya ukusanyaji mapato katika halmashauri; kutoa semina kwa maafisa ugani, watumishi wa afya na mabaraza ya ardhi; pamoja na kufuatilia matumizi ya fedha katika halmashauri zote za Iringa.
Swella ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa, akisisitiza kuwa kuzuia rushwa ni jukumu la kila mmoja na kila mmoja anatakiwa kutimiza wajibu wake.




