Na Mwandishi Wetu
Mgogoro wa kisheria unaohusisha ununuzi wa ardhi yenye thamani ya Sh bilioni 1.6 umeibuka na kumfikisha mikononi mwa Jeshi la Polisi aliyewahi kuwa Mbunge wa Korogwe Mjini, Yusuph Abdallah Nassir, kwa mahojiano kuhusu tuhuma za kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu.
Mbunge huyo mstaafu alishikiliwa kwa saa kadhaa na Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam kabla ya kuachiwa kwa dhamana huku uchunguzi ukiendelea.
Chanzo cha sakata hilo ni makubaliano ya kibiashara yaliyofikiwa Machi 2024 kati yake na kampuni ya ATN Petroleum Limited, ambapo inadaiwa alikabidhiwa fedha hizo kwa ajili ya kununua hekari 200 za ardhi eneo la Chongoleani, mkoani Tanga, kwa lengo la uwekezaji katika sekta ya mafuta.
Hata hivyo, wakili wa kampuni hiyo, Fatuma Mwaja, amedai kuwa badala ya ardhi hiyo kuandikishwa kwa jina la ATN Petroleum kama ilivyokubaliwa, hati ilitolewa kwa jina la kampuni ya Black Gold Oil and Gas Ltd, inayodaiwa kumilikiwa na mtuhumiwa.
Kwa mujibu wa maelezo ya wakili huyo, ATN ilikuwa na mpango wa kujenga matanki ya kuhifadhia mafuta karibu na mradi wa bomba la mafuta, hatua ambayo ingetengeneza ajira na kuchochea uwekezaji. Ndoto hiyo imekwama kufuatia sintofahamu ya umiliki wa ardhi husika.
Inadaiwa pia kuwa baada ya kuzuka kwa mgogoro huo, hatua zilichukuliwa kwa kuandikiwa barua Msajili wa Hati Mkoa wa Tanga kuomba hati hiyo ifutwe. Serikali ya Mkoa kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali iliitisha kikao cha usuluhishi Februari 18 mwaka huu, lakini pande hizo hazikufikia mwafaka.
Kwa upande wake, Nassir amekiri kuwepo kwa mgogoro kati yake na ATN na kueleza kuwa suala hilo limesharejeshwa kwa Mwanasheria wa Mkoa wa Tanga kwa hatua zaidi za kisheria, akisisitiza hawezi kulizungumzia kwa undani kwa sasa kwa kuwa liko kwenye vyombo vya sheria.
Kwa sasa, shauri hilo lipo katika hatua za upelelezi Polisi, huku hatua za kisheria zikisubiriwa baada ya uchunguzi kukamilika.




