Mwanariadha wa mbio ndefu wa Tanzania, Gabriel Gerald Geay, ameendelea kuipeperusha vyema bendera ya Taifa baada ya kuibuka mshindi katika mashindano ya Daegu Marathon yaliyofanyika nchini Korea Kusini, mafanikio yanayoendelea kuonesha ushupavu wa wanamichezo wa Kitanzania katika jukwaa la kimataifa.

Akizungumza leo, tarehe 26/02/2026, katika hafla fupi ya kumpokea bingwa wa Daegu Marathon, Gabriel Gerald Geay, iliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Jasmine Kikwete, Balozi wa Jumuiya ya Madola wa Utalii na Uwekezaji, ameipongeza TANAPA kwa maono ya kuwafadhili wanariadha. Alibainisha kuwa kupitia mashindano hayo yanayofuatiliwa duniani, nembo na ujumbe wa Hifadhi za Taifa umefika mbali zaidi.

Kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Arusha, Witness Shoo, amempongeza Geay kwa kutetea taji lake la ushindi wa kwanza na kuiletea Tanzania medali ya dhahabu alibainisha kuwa kabla ya safari yake kuelekea mashindano ya Daegu Marathon, Geay alitembelea Hifadhi ya Taifa Arusha na kupewa baraka zote linalodhihirisha uhusiano chanya kati ya Utalii na michezo

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Biashara TANAPA, Jully Bede Lyimo, ameeleza kuwa TANAPA inatambua mchango wa zao la utalii wa michezo kwenye kuongeza idadi ya watalii na mapato katika Hifadhi zake na Shirika linaendelea kukuza utalii wa michezo na kutumia wanariadha wa kimataifa katika kutangaza Hifadhi za Taifa na Utalii wa nchi yetu ya Tanzania

Kwa upande wake, Gabriel Gerald Geay ameishukuru TANAPA kwa kuunga mkono wanamichezo na kutoa wito kwa wadau wengine kusaidia vipaji vya vijana.

Katika Daegu Marathon, Tanzania imeandika historia kwa kupata washindi watatu kwa mara ya kwanza: Gabriel Gerald Geay (nafasi ya kwanza), Emmanuel Dinday (nafasi ya tatu) na Bernard Geay (nafasi ya kumi na moja).

Ushindi huu unaonesha wazi kuwa uwekezaji katika michezo ni nyenzo madhubuti ya kuitangaza Tanzania kimataifa.