Kamanda wa Polisi Mkoani  Ruvuma SACP Marco Chillya,akionyesha uwezo wa kucheza mpira kabla ya kufungua mashindano ya Wailes Super Cup  kwa shule za Sekondari katika Halmashauri ya Mji Mbinga.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Wailes Frank Ndunguru kushoto,akimpa zawadi ya jeshi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma SACP Marco Chillya,kabla ya  ufunguzi wa mashindano ya Wailes Super Cup yanaoendelea katika uwanja wa michezo CCM Mbinga.

…….

Na Mwandishi Wetu, Mbinga

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Ruvuma SACP Marco Chillya,amezindua rasmi mashindano ya Wailes Super Cup kwa wanafunzi wa shule nane za sekondari katika Halmashauri ya Mji Mbinga yaliyoandaliwa na Kampuni ya Wailes kwa lengo la kusaka vipaji kwa vijana.

Akizungumza baada ya kuzindua mashindano hayo kamanda Chillya amewasisitiza vijana hao kutumia michezo hiyo kuonyesha vipaji vyao ili vitambuliwe na wadau  wengi zaidi wa mpira wa miguu wa ndani na nje ya nchi pamoja na kudumisha amani na utulivu hapa nchini.

Chillya alisema,kwa sasa michezo ni ajira kubwa kwani hata wachezaji hususana wa mpira wa miguu wanalipwa fedha nyingi ikilinganisha na watumishi wa Serikali,hivyo vijana watumie nafasi hiyo kufanya vizur kwa kuonyesha vipaji vyao  ili kuvutia za ligi kuu zikiemo Simba na Yanga.

“michezo ni  furaha na amani,kama kusingekuwa na amani basi mashindano haya yasingekuwepo,nawaomba sana vijana tumieni mashindano haya kuonyesha vipaji huku mkizingatia suala la kudumisha amani ya nchi yetu”alisema Kamanda Chillya.

Kamanda Chillya,amempongeza Frank Ndunguru,kuwa na wazo la kuanzisha michezo hasa mpira wa miguu  kwa shule za Sekondari Wilayani Mbinga,hata hivyo ameshauri kupeleka mashindano  michezo hiyo kwenye  Halmashauri nyingine za Mkoa wa Ruvuma ili vijana wengi zaidi wapate fursa ya kuonyesha vipaji vyao.

Mratibu wa mashindano hayo Ahmad Mwalimu alisema,hii ni mara ya kwanza Kampuni ya Wailes yenye makao makuu katika mji wa Mbinga kuanzisha mashindano ya mpira wa miguu kwa shule za sekondari Wilayani Mbinga.

Alisema,Kampuni ya Wailes inayojihusisha zaidi na biashara ya nguo,vifaa vya shule na maofisini na kuandaa matangazo mbalimbali ndiyo maana imeandaa michezo hiyo ili iwe sehemu ya kutangaza kampuni  na huduma inazotoa.

“Sisi kama Wailes tukaona kuwa ili biashara yetu  iweze kufanya vizuri tunahitaji watu ambao watahusika moja kwa moja kuzifikia biashara zetu,kwa hiyo  tukaangalia makundi yote ya kijamii na wiki iliyopita tumefungua mashindano kama haya kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga kule kata ya Mapera”alisema Mwalimu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Wailes Frank Ndunguru alisema,mashindano haya ya Wailes Super Cup yanashilikisha jumla ya shule za sekondari nane ikiwemo shule ya kutwa Mbinga,Ruhuwiko na Makita na mashindano hayo yatahitimishwa tarehe 6 Machi.

“Mashindano yetu haya yanaongozwa chini ya Kauli Mbiu isemayo, Tanzania  yetu Amani yetu kuwa Mzalendo Dumisha Amani,kwa hiyo sisi sote tutaendelea kudumisha Amani ili kuwa na Tanzania salama yenye utelivu mkubwa”alisema Ndunguru.

Kwa upande wake Afisa Michezo wa Halmashauri ya Mji Mbinga Jackson Moyo alisema,michezo hiyo kwa shule za Sekondari za Halmashauri ya Mji Mbinga yatasaidia sana kuibua na kukuza vipaji vya vijana na hivyo kupata timu itakayofanya vizuri kwenye mashindano ya shule za Sekondari(Umiseta).

Katika mchezo wa ufunguzi,Timu ya shule ya sekondari Mbinga(Mbinga Day)iliibuka mshindi baada ya kuifunga shule ya Sekondari Ruhuwiko goli 1-0.