Mkuu wa Chuo cha Veta Songea Mkoani Ruvuma Rahabu Mwakatundu, akionyesha baadhi ya vifaa vinavyotumika kufundisha wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho.
Baadhi ya Wanafunzi wa fani ya umeme wa majumbani wakiendelea na mafunzo yao.
……………..
Na Mwandishi Wetu, Songea.
KATI ya wasichana 430 kutoka Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma,waliotakiwa kujiunga na chuo cha ufundi veta Songea kwa ufadhili wa Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania(TACAIDS) chini ya mradi wa Timiza Malengo, ni wasichana 27 ndiyo waliojiunga na chuo hicho kwa muhula wa masomo 2026.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo hicho Rahabu Mwakatundu,wakati akitoa taarifa ya kozi na miradi mbalimbali inayotekelezwa na chuo hicho kwa muhula wa masomo ulioanza Mwezi Januari mwaka 2026.
Alisema,licha ya Serikali kutoa fursa kwa wasichana hao kujiunga na Veta,hata hivyo kumekuwa na ugumu kuwapa kwa ajili ya kuwapa ujuzi utakaowasaidia kujiajiri au kuajiriwa ili kujipatia kipato baada ya kumaliza mafunzo yao.
“Lengo la mradi wa Timiza malengo ni kuwaepusha vijana wa kike kuingia katika hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo ukimwi na biashara ya ngono”alisema Mwakatundu.
Alitaja muda wa kozi hiyo ni miezi mitatu ambapo mabinti wanachagua fani yoyote wanayoipenda na walengwa wakubwa ni mabinti wanaotoka katika mazingira hatarishi na kaya masikini.
Alisema,hata hivyo imekuwa vigumu kuwapata vijana hao kwani wanapotafutwa wengi hawako tayari kwenda kujiunga na chuo na wengine wamejiingiza kwenye shughuli nyingine.
“Tayari tumewasiliana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Mbinga ilitusaidie kuwapata vijana hao,inasikitisha kuona Serikali imeleta fursa inayotolewa bure, lakini vijana wameshindwa kuchangamkia”alisema Mwakatundu.
Alisema,Veta Songea imepangiwa kupokea jumla ya vijana wa kike 5,000 kwa ajili ya kupata mafunzo lakini changamoto kubwa ni mwitio mdogo wa vijana wenyewe kujiunga na chuo.
Amewataka wazazi na walezi Mkoani Ruvuma, kupeleka watoto wao wa kike katika chuo hicho ili waweze kupata elimu na ujuzi utakaowawezesha kuwa wataalam wa fani mbalimbali na kutimiza ndoto zao badala ya kuwaacha mitaani.
“Wazazi na walezi wahamasishe watoto wao hasa wa kike kuja kupata mafunzo ya ufundi stadi kwani sera ya uchumi wa viwanda inahitaji wataalam wengi,hivyo juhudi zinahitajika kuwahamasisha watoto hawa kwa manufaa yao,familia na Taifa kwa ujumla”alisema Mwakatundu.
Kwa mujibu wa Mwakatundu,Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya elimu imefanya uwekezaji mkubwa wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwa ajili ya kutoa elimu bora ya ufundi kwa vijana lengo ni kupunguza utegemezi ili wanapomaliza waweze kujitegemea kwa kujiajiri au kuajiriwa.
Mwakatundu alisema,ni muhimu wazazi wapeleke watoto katika chuo cha Veta Songea kwani kutokana na umuhimu wa ufundi, Serikali imewekeza nguvu kubwa ya vifaa na walimu ili kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata ujuzi utakaomsaidia kujikomboa kiuchumi.
Mwakatundu alitaja mradi mwingine, ni Wanawake na Samia unaohusisha wanawake wote wa Mkoa wa Ruvuma kujiunga na Veta ili kupata ujuzi na watakapomaliza waweze kumudu maisha yao.
Alisema,kupitia mradi huo mwitikio wa wanawake kujiunga na Veta ni mkubwa na wengi waliomaliza wamejiajiri kupitia fani mbalimbali na mradi utaendelea kupokea wanawake katika awamu ya pili mwezi Machi mwaka huu.
Anawahamasisha wanawake wa Mkoa wa Ruvuma,kujiunga na Taasisi ya Wanawake na Samia,ili wapate fursa ya kujiunga na Veta na kupata mafunzo ya ufundi katika fani mbalimbali yanayotolewa bure chini ya ufadhili wa Taasisi hiyo.
Mwanafunzi wa mwaka wa pili fani ya umeme wa majumbani Shafi Milongo,ameishukuru Serikali kupitia mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi(Veta)kutoa nafasi kwa vijana kujiunga na Veta Songea kwani itawasaidia kupata ujuzi na hatimaye waweze kujitegemea kwenye maisha yao.




