DENIS MLOWE IRINGA
HAFLA ya utoaji wa viungo saidizi kwa watu wenye ulemavu wa mkoa wa Iringa imefanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa mnamo tarehe 23 Februari 2026, huku viongozi mbalimbali wakihudhuria na kutoa salamu za matumaini kwa jamii.
Hafla hiyo imeandaliwa na Taasisi ya Ritta Kabati Trust Fund iliyo chini ya Mbunge wa Jimbo la Kilolo Ritha Kabati aliyogharamia utengenezaji wa viungo saidizi vya wahitaji 13 vyenye thamani zaidi ya milioni 20.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kilolo John Kiteve alitoa pongezi kwa wabunge na viongozi wanaoweka maslahi ya wananchi mbele, akimsifu mbunge wa Kilolo, Dkt. Ritta Kabati, kwa moyo wake wa kujitoa katika kuhudumia watu wenye uhitaji. Alisema kuwa uongozi wa kweli hupimwa kwa jinsi kiongozi anavyogusa maisha ya watu anaowaongoza.
Katika hotuba yake, Kiteve alisisitiza kuwa kazi ya kuwahudumia watu wenye ulemavu si ya serikali pekee, bali inahitaji moyo na wito wa kibinadamu.
Alimtaja Dkt. Kabati kama mtu mwenye “human factor” inayohitajika katika kutoa huduma zenye kugusa maisha ya watu hata kabla ya tiba kutolewa.
Kwa upande wake, Dkt. Kabati, ambaye pia ndiye mwanzilishi wa Ritta Kabati Trust Fund, alieleza kuwa taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele kuwasaidia wananchi wenye uhitaji tangu mwaka 2020. Tangu kuanzishwa kwake, taasisi tayari imeshawawezesha zaidi ya watu 300 kupitia huduma za kijamii, msaada wa vifaa saidizi na kampeni za uhamasishaji.
Dkt. Kabati aliongeza kuwa hafla ya mwaka huu imeratibiwa mahsusi katika kipindi cha wiki ya wanawake, ikiwa ni sehemu ya mchango wa wanawake katika kutoa huduma za huruma kwa jamii. Alisema kuwa watu wenye ulemavu bado wanakabiliwa na changamoto za kifedha, vifaa saidizi na upatikanaji wa huduma rafiki, hivyo kuahidi kuendelea kutafuta wadau zaidi ili kufikia walengwa wengi.
Akitoa taarifa ya maandalizi, Katibu wa Mbunge, Akida Khalfan, alisema kuwa mwaka huu watu 13 wamepatiwa viungo saidizi ambavyo tayari vimetengenezwa kufikia mahitaji yao mahsusi. Alisisitiza kuwa bado uhitaji ni mkubwa, hivyo aliwasihi wadau na taasisi mbalimbali kuendelea kutoa mchango wao.
Katika salamu zake, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Estomin Kyando ambaye alikuwa mgeni rasmi alimshukuru mbunge na Hospitali ya Rufaa ya Iringa kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha watu wenye ulemavu wanahudumiwa ipasavyo.
Alisema kuwa juhudi hizi ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na dira ya kitaifa ya kuwatambua watu wenye mahitaji maalum.
Aidha, Kyando alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa kipaumbele kwa makundi maalum, ikiwemo bima ya afya kwa wananchi wasiojiweza na maboresho ya huduma za afya kwenye maeneo ya pembezoni.
Alisema hatua hizi zimeanza kuleta mabadiliko makubwa katika wilaya ya Kilolo.
Akizungumza katika hafla hiyo Mganga mfawidhi wa hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa Dr.Alfred Mwakalebela ameshukuru taasisi hiyo kwa ushirikiano mkubwa na hospitali hiyo akitaka wadau wengine kuendelea kushirikiana ili kuweza kuwa na maendeleo ya pamoja katika sekta ya afya.
Wazungumzaji mbalimbali walitoa shukrani kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kwa kushiriki kikamilifu katika upimaji na utengenezaji wa viungo saidizi. Hospitali hiyo imetajwa kuwa kiungo muhimu katika kuhakikisha huduma hizi zinapatikana kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Kwa niaba ya waliokabidhiwa viungo Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu mkoa wa Iringa (SHIVYAWATA) Shaban Shomari wameeleza furaha yao, wakisema kuwa viungo bandia vitawasaidia kurejea kwenye shughuli za kiuchumi na kijamii.
Alisema kuwa miaka mingi walikuwa hawana uwezo wa kufanya kazi za msingi kutokana na ulemavu, lakini sasa wanayo matumaini mapya.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa makabidhiano rasmi ya vifaa, sala za shukrani na ahadi za kuendelea kufanya kazi kwa pamoja kati ya serikali, taasisi binafsi na wadau wa maendeleo. Washiriki wote walikubaliana kuwa juhudi hizi zinapaswa kuendelezwa ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika safari ya maendeleo.





