Na. John Bukuku – Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Waziri Rajabu, Februari 19, 2026 ametembelea Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) lililopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam, na kufanya kikao na Baraza la shirika hilo kwa lengo la kujadili maboresho ya utendaji kazi.
Akizungumza mara baada ya kikao hicho, ametoa maelekezo kwa shirika hilo kufanya marekebisho ya sera (addendum) ili kuanza mwelekeo wa uwekezaji na kuvutia wawekezaji badala ya kuendelea na mfumo wa uzalishaji kama ulivyokuwa tangu kuanzishwa kwake.
Aidha, amebainisha kuwa TIRDO ina maeneo yenye fursa kubwa za kiuchumi na inapaswa kuwa na sera itakayowezesha kushirikiana na wawekezaji katika biashara na maendeleo ya viwanda.
Katika ziara hiyo, Bw. Waziri ametembelea miradi mbalimbali, ikiwemo jengo la utawala ambalo limechukua muda mrefu kukamilika.
Amesema kuwa Wizara, kwa kushirikiana na SIDO, itafanya tathmini upya ya mradi huo ili kubaini kama unafaa kuendelea au kufanyiwa maboresho kulingana na mahitaji ya sasa, akieleza kuwa ramani iliyotengenezwa miaka arobaini iliyopita huenda isikidhi mahitaji ya sasa ya taasisi.
Pia ametembelea vituo vya ubunifu (incubators) vya vijana wa ICT, uzalishaji wa vyakula na madawa, pamoja na eneo la ubunifu wa utengenezaji wa magari ya umeme. Amesema kuwa amefurahishwa na mapinduzi makubwa ya ubunifu aliyoyaona, hususan katika utengenezaji wa magari ya umeme yenye uwezo wa kutembea hadi kilomita 150 kwa chaji moja.
Amesema kuwa Wizara itaendelea kutoa sapoti kwa wabunifu na wafanyabiashara ili waweze kuendeleza miradi yao.
Akizungumzia ubunifu unaofanywa na Watanzania kupitia KP, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri, amesema:
“Nimeona mapinduzi makubwa sana ya uzalishaji na ubunifu wa magari ya umeme. Kwa kweli sisi Wizara ya Viwanda na Biashara lazima tumpe sapoti. Ametoa zake nyingi sana za mfukoni, kachoka, anahitaji tumpe sapoti kubwa sana na nielekeze TBS na TIRDO. Tarehe 28/02/2026 waje Dodoma ofisini tuje kuzungumzia suala la namna gani wabunifu wa namna hii wa aina ya kina KP tunaweza tukawasaidia,” amesema Balozi Waziri.
Aidha, Balozi Waziri amesisitiza kuhusu uwezo wa gari hilo la umeme, akiongeza:
“Lakini ukiangalia gari tayari na mteja kasha lipia, ina maana kwamba huyu akipata fursa anaweza ikawa ndiyo Keep Motors za hapa mjini na unataka kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Gari hiyo peke yake ikishakuwa na chaji inatembea kilomita mia moja hamsini. Si ndiyo mtu anazunguka Dar es Salaam nzima hapa mjini? Tunahitaji kuwapa sapoti,” amesema Balozi Waziri.
Katibu Mkuu pia ametoa wito kwa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kujitangaza zaidi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ili wananchi waweze kufahamu kazi kubwa inayofanywa na taasisi hizo.
Pia, amewataka watumishi wa Wizara na taasisi zake kubadilika na kuhakikisha wanakuwa wezeshi wa biashara na viwanda badala ya kuwa vikwazo, akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa weledi na utu ili kufanikisha azma ya kukuza viwanda na biashara nchini.




