Na Silivia Amandius.
Bukoba.
Zoezi la usajili wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa wafanyabiashara, kurasimisha biashara pamoja na kufanya makadirio ya kodi limefanyika katika Kata ya Rwamishenye eneo lenye wafanyabiashara wakubwa na wadogo ndani ya Manispaa ya Bukoba.
Zoezi hilo limefanyika Leo feb 18, 2026 ambapo lilihusisha utoaji wa elimu kupitia Dawati la Uwezeshaji Biashara ili kuwajengea wafanyabiashara uelewa sahihi kuhusu masuala ya kodi na uendeshaji wa biashara zao kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Agnesi Kimbondile, Mkuu wa Kitengo cha Dawati la Uwezeshaji Biashara, amesema kuwa lengo kuu la kutoa elimu hiyo ni kuwawezesha wafanyabiashara kuelewa wajibu wao wa kulipa kodi, kufahamu taratibu za usajili wa biashara na TIN, pamoja na kuwasaidia kufanya makadirio sahihi ya kodi ili kuepuka migogoro na adhabu zisizo za lazima.
Aliongeza kuwa elimu hiyo inalenga pia kuongeza wigo wa walipa kodi kwa kuhamasisha wafanyabiashara ambao bado hawajasajiliwa kuingia rasmi katika mfumo wa kodi, hatua ambayo itawawezesha kupata fursa mbalimbali ikiwemo mikopo, kushiriki zabuni za Serikali na kupata huduma nyingine muhimu za kifedha na kibiashara.
Kwa upande wao, wananchi na wafanyabiashara waliopata huduma hiyo waliishukuru Serikali na Dawati la Uwezeshaji Biashara kwa kuwaletea elimu hiyo karibu na maeneo yao, wakisema kuwa imewasaidia kufahamu haki na wajibu wao, pamoja na kuwajengea ujasiri wa kuendesha biashara zao kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.
Wafanyabiashara hao pia walieleza kuwa zoezi hilo limeondoa hofu na mkanganyiko waliokuwa nao kuhusu masuala ya kodi, na kwamba sasa wanaelewa namna bora ya kukadiria na kulipa kodi zao kwa wakati, hali itakayosaidia kukuza biashara zao na kuchangia maendeleo ya Manispaa ya Bukoba.





