NA FAUZIA MUSSA
Mashindano ya gofu ya Valentine’s Golf Challenge – 18 Holes Stableford Competition yamefanyika katika viwanja vya Seacliff yakiwakutanisha wachezaji mbalimbali katika siku maalum ya wapendanao, huku ushindani mkali ukishuhudiwa katika mashimo yote ya uwanja huo.
Mashindano hayo yaliyofadhiliwa na United Petroleum, Villa Kiva, Mpola Halisi Coffee, Zanzi Resort, ZMMI na Digilinks, yalianza rasmi saa 11:00 jioni kwa kundi la kwanza huku washiriki wakitakiwa kuripoti dakika 10 kabla ya muda wao wa kuanza kwa ajili ya maandalizi na ukaguzi wa mwisho wa vifaa.
Kwa mujibu wa ratiba ya droo, wachezaji walipangwa katika makundi tofauti wakishindana kwa mfumo wa 2-ball better ball, ambapo kila mchezaji alicheza mpira wake lakini timu ilihesabiwa kwa alama bora kati ya wachezaji wawili katika kila shimo.
Akizungumza kandoni mwa mashindano hayo, Meneja wa Gofu, Sophie Nyanjera, alisema lengo la mashindano hayo ni kuendeleza mchezo wa gofu pamoja na kuhamasisha ushiriki wa jamii katika mchezo huo.
“Lengo la tukio hili ni kukuza mchezo wa gofu na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wanachama na wadau. Tunataka kuona gofu inakuwa mchezo wa watu wengi zaidi. Mashindano haya ya Valentine yameleta wachezaji kutoka maeneo tofauti na yameongeza ushindani na urafiki kwa wakati mmoja,” alisema Sophie.
Kwa mujibu wa mfumo wa mashindano wa 2-ball better ball, kila timu iliundwa na wachezaji wawili huku kila mmoja akicheza mpira wake. Alama ya timu ilichukuliwa kutoka kwa mchezaji aliyepata matokeo bora katika kila shimo, jambo lililoongeza msisimko na mikakati ya pamoja uwanjani.
Baadhi ya washiriki walisema mfumo wa better ball umeongeza msisimko kwani unahitaji ushirikiano wa karibu baina ya wachezaji wawili katika kila timu. Walisema ushindani ulikuwa wa hali ya juu na ulihitaji umakini mkubwa.
“Ni mashindano yanayohitaji nidhamu na mawasiliano mazuri kati ya wachezaji wa timu moja. Kila shimo linaweza kubadilisha matokeo, hivyo unalazimika kupambana hadi mwisho,” alisema Shemndolwa, mmoja wa washiriki.
Tukio hilo limeendelea kudhihirisha kuwa gofu si mchezo wa ushindani pekee, bali pia ni jukwaa la kukuza mahusiano na kuimarisha afya kupitia michezo.




