Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Alnason Nguvila akizungumza katika halfa hiyo jijini Arusha leo

…………
Na Happy Lazaro, Arusha .
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Alnason Nguvila, amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote, kuhakikisha wanatenga bajeti ya kutekeleza shughuli za utalii kwenye maeneo yao, kubuni vyanzo vya mapato pamoja na kusimamia ukusanyaji wa mapato, ikiwa ni pamoja na kutoka maofisini na kuwafuata wananchi ili kubaini changamoto zao na kuzitatua kwa haraka.
Dkt.Nguvila ameyasema hayo leo wakati akizungumza na baadhi ya watumishi wa Umma mkoa wa Arusha, kwenye hafla fupi ya mapokezi yake, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa muda mfupi baada ya kupokelewa ofisini hapo, tayari kwa kuanza kutekeleza majukumu yake, kwa washifa huo.
Aidha ametoa msisitizo kwa watumishi wa Umma kufanya kazi kwa kufuata Sheria, Taratibu na Kanuni kwa kuzingatia kiwango cha juu cha Maadili ya Utumishi wa Umma ili kufikia lengo la Serikali la kuwahudumia wananchi.
Amewataka watumishi hao, kila mmoja kwa nafasi yake kuzingatia kuwa, mkoa wa Arusha ni mkoa wa Utalii hivyo kuhakikisha wadau wote wa utalii wanafanya kazi kwenye mazingira rafiki yasiyo na vikwazo vya aina yoyote huku akisisitiza kuto kuvumilia vikwazo vya kiutendaji wala urasimu unaokwaza wawekezaji katika sekta ya utalii.
“Mkoa wa Arusha unapaswa kuimarika zaidi katika sekta ya utalii, kwa kuwa kila wilaya ina vivutio vyake, hivyo si busara kwa baadhi ya watendaji kuweka urasimu usio wa lazima unaoweza kudhoofisha sekta hiyo, sitavumilia urasimu wala migogoro inayokwamisha wawekezaji katika sekta ya utalii”. Amesema Dkt.Nguvila.
Katika kutekeleza maelekezo ya Serikali, Dkt.Nguvila ameataka viongozi hao, kuwa na kampeni maalumu ya kutoa elimu na usajili sambamba na kuhamasisha wananchi kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa wote, ili ili kufikia lengo la Serikali ya awamu ya sita ya kila mwananchi kujiunga na Bima hiyo, itakayowawezesha kupata huduma za matibabu wanapougua.
Aidha Dkt.Nguvila amemshukuru Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kumuanini na kumteua kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha na ameahidi kushirikiana na watalamu wa ngazi zote katika kuwahudumi wananchi.



