Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akizungumza kwenye mahafali hayo jijini Arusha leo
Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA)Prof.Eliamani Sedoyeka akizungumza kwenye mahafali hayo yaliyofanyika katika hotel ya Ngurdoto iliyopo mkoani Arusha
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Waziri wa fedha Balozi Khamis Omar Mussa amewataka wanafunzi na wahitimu wa Shahada ya Uzamili kuimarisha zaidi tafiti zao za kitaalumakwani Tafiti hizo zinapaswa kuelekezwa katika kutoa majibu ya changamoto halisi zinazoikabili jamii na Taifa letu, ikiwemo masuala ya usimamizi wa fedha za umma, ukuaji wa uchumi jumuishi, ajira, ubunifu, na matumizi sahihi ya teknolojia.
Aidha ametaka Tasnia hizo ziwe chachu ya sera bora, maamuzi sahihi na maendeleo endelevu kwa wananchi na Taifa letu.
Hayo yasemwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), wakati akihutubia kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), katika Mahafali ya 27 (Duru ya Pili) ya Chuo hicho, yaliyofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto, mkoani Arusha.
Amesema kuwa ,ni jambo la kujivunia kuona IAA ikiendelea kuboresha na kuimarisha mifumo yake ya ufundishaji na ujifunzaji, hususan kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili. Matumizi ya mfumo wa ana kwa ana darasani sambamba na mfumo wa mtandaoni (online).
,Mfumo huu umeongeza upatikanaji wa elimu, kuboresha ubora wa ufundishaji, na kuwapa wanafunzi unyumbufu unaoendana na mazingira ya kazi na maendeleo ya teknolojia ya kisasa, ambapo huo ni ushahidi wa wazi kuwa Chuo kinaendana na mabadiliko ya dunia ya sayansi na teknolojia.
Mchango wa Chuo cha Uhasibu Arusha katika uchumi wa Taifa letu hauwezi kupuuzwa. IAA imeendelea kuzalisha wataalam wa fedha, uhasibu, uchumi, kodi, utalii, usimamizi biashara, benki, ununuzi na ugavi, masoko, bima, TEHAMA na nyingine nyingi; ambao wamekuwa mhimili muhimu katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, usimamizi wa fedha za umma, sekta binafsi, taasisi za kifedha na miradi ya maendeleo. Kupitia wahitimu wake, Chuo kimechangia kwa vitendo katika kukuza uwajibikaji, uwazi na nidhamu ya kifedha nchini.
“Miongoni mwa vichocheo vya kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025-2050 ni Mageuzi ya Kidigitali na Utafiti na Maendeleo. Niwapongeze Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa kuweka mipango na mikakati ya kuboresha na kuongeza ufanisi kwenye utoaji wa mafunzo, ushauri wa kitaalam na ufanyaji wa tafiti; inayotembea kwenye maono ya Taifa “amesema Naibu Waziri Laurent Luswetula.
“Mageuzi ya Kidigitali ni kichocheo muhimu cha maendeleo hususani katika kuboresha ukuaji wa uchumi na kuimarisha huduma za jamii ikiwemo elimu. Serikali inatambua na kupongeza juhudi za IAA katika kuwekeza kwenye mifumo ya kidigitali. Mipango ya kuboresha miundombinu ya TEHAMA,
“mifumo ya kujifunzia kwa njia ya mtandao, usimamizi wa kitaaluma na huduma za wanafunzi ni nguzo muhimu katika kuongeza ufanisi na ushindani wa Chuo kitaifa na kimataifa. Wizara ya Fedha itaendelea kushirikiana na Chuo katika kuwezesha upatikanaji wa rasilimali na mazingira rafiki ya kifedha yatakayosaidia utekelezaji wa mipango hii ya kidigitali.”amesema .
Amesema kuwa katika nchi yoyote yenye dhamira ya maendeleo ya kweli kama ilivyo kwa nchi yetu ya Tanzania, Utafiti na Maendeleo ni nyenzo muhimu katika kuongeza ubunifu, kutatua changamoto, kuongeza tija katika uzalishaji na kutoa mwongozo katika uundaji wa sera mbalimbali.
“Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya ukuaji wa uchumi, uimarishaji wa nidhamu ya fedha za umma, na maendeleo jumuishi yanayomgusa kila Mtanzania.”amesema .
“Katika muktadha huo, sekta ya fedha, uhasibu, uchumi, benki, usimamizi wa biashara, usimamizi wa miradi, ununuzi na ugavi, usimamizi wa rasimali watu, uongozi na utawala na nyingine zinazotolewa katika ngazi ya Shahada ya Uzamili (Master’s Degree) ni nguzo muhimu sana katika kuhakikisha rasilimali za Taifa zinakusanywa, zinapangwa, zinatumika na zinadhibitiwa kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji.”amesema .
“Niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu, ikiwemo IAA, ili mitaala iendelee kuendana na mahitaji halisi ya soko la ajira na mabadiliko ya uchumi wa kkidijitali”amesema Balozi Khamis .
Ameongeza kuwa Wizara ya Fedha itaendelea kuunga mkono Chuo cha Uhasibu Arusha katika kutekeleza majukumu yake ya msingi. Wizara itaendelea kushirikiana na Chuo katika kuboresha mazingira ya ufundishaji na utafiti, kuimarisha ushirikiano na taasisi za fedha na uchumi, pamoja na kuwezesha Chuo kushiriki kikamilifu katika miradi ya kimkakati ya Taifa inayohusiana na maendeleo ya rasilimali watu na uchumi wa nchi.
Naye Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA)Prof.Eliamani Sedoyeka akizungumza kwenye mahafali hayo amesema kuwa,, Leo ni siku muhimu kwa Chuo chetu, kwani tunashuhudia matunda ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Chuo pamoja na Serikali katika elimu ya juu, hususani katika programu za Shahada ya Uzamili zinazolenga kuandaa viongozi, wataalam, na wasomi watakaobeba dira ya maendeleo ya Taifa la Tanzania.
Amesema kuwa, Jumla ya Wahitimu ni 2,250 kati yao wanaume ni 1,369 sawa na asilimia 60.8 na wanawake ni 881 sawa na asilimia 39.2 .
Ameongeza kuwa ,chuo cha Uhasibu Arusha wanajivunia kuwa miongoni mwa taasisi za elimu ya juu nchini zinazotekeleza mwelekeo wa Kitaifa wa kupanua upatikanaji wa elimu ya juu kwa kuanzisha na kuimarisha mfumo jumuishi wa utoaji wa shahada ya Uzamili (Master’s degree) unaochanganya masomo ya ana kwa ana darasani (Physical classes) na ya mtandaoni kwa wakati mmoja yaani ‘blended mode’.
Mfumo huu unaendana kikamilifu na sera za taifa za matumizi ya TEHAMA katika elimu, na umewezesha wataalam walioko katika maeneo mbalimbali ya nchini kuendelea na masomo bila kuathiri majukumu yao ya kazi na huduma kwa jamii.
“Kupitia mfumo huu bunifu, Chuo kimeongeza wigo wa upatikanaji wa elimu ya Uzamili, kuboresha ubora wa ujifunzaji, na kuendana na mabadiliko ya dunia ya kazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.”amesema Prof .Sedoyeka .
“Chuo cha Uhasibu Arusha tunatoa Shahada yetu ya Uzamili kwa namna ya tofauti na ya kipekee kabisa. Tofauti ya kipekee ya Shahada ya Uzamili ya IAA ikilinganishwa na vyuo vingine vingi ni muda wa masomo,ambapo programu zetu zinakamilika kwa mwaka mmoja bila kupunguza viwango vya kitaaluma, ubora wa utafiti, wala maadili ya elimu ya juu.”amesema Prof Sedoyeka.
Amesema kuwa muda huu ni mfupi lakini wenye tija umewezekana kutokana na upangaji makini wa mitaala, usimamizi thabiti wa masomo, tathmini endelevu, na nidhamu ya hali ya juu ya kitaaluma kwa wanafunzi na wahadhiri wetu, sambamba na miongozo ya kitaifa ya elimu.




