Na Timothy Mwakyenda- MAELEZO
Serikali imesajili zaidi ya Anwani za Makazi Milioni 12.9 ili kuyatambua maeneo mbalimbali na kuyarasimisha kwenye mfumo wa kidijitali.
Takwimu hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Nicholas Merinyo Mkapa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Bw. Mohamed Hamis Abdullah leo Februari 6, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere kilichopo jijini Dar es salaam ikiwa ni mwendelezo wa Kongamano la Anwani za Makazi na Maonesho ya Teknolojia ya Huduma za Posta.
“Tanzania ilianza mchakato wa usajili wa Anwani za Makazi nchi nzima tangu mwaka 2010, hadi kufikia mwaka 2026 imefanikiwa kusajili zaidi ya anwani milioni 12.9”, amesema Naibu Katibu Mkuu, Mkapa.
Naibu Katibu Mkuu Mkapa ameongeza kuwa, Anwani za Makazi ni kitovu cha maendeleo kwa nchi kwa sababu zinatambua na kuunganisha maeneo mbalimbali ya nchi na kuziweka pamoja katika mfumo wa kidijitali ambapo toka zoezi la usajili lianze, jumla ya mifumo 29 imeunganishwa ikiwemo Shirika la Posta.
Ametoa rai kwa washiriki wa kongamano hilo kuwa katika siku za majadiliano, wajumbe waweke mkazo katika kujadili namna ambavyo Anwani za Makazi zina umuhimu katika utoaji wa huduma za afya, elimu na kukuza uchumi.
Aidha, Mkapa amesisitiza kuwa mifumo imara ya Anwani za Makazi huimarisha utu wa watu na kuibua fursa za kimaendeleo kwa watu wote.




