Na John Bukuku, Dar es Salaam

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanya ukaguzi wa kitaalamu wa mita za umeme kufuatia malalamiko ya baadhi ya wateja kuhusu umeme kuisha haraka bila sababu ya msingi.

Malalamiko hayo yaliibuliwa na wananchi kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, wakidai kuwa mita zao zina kasoro za kiutendaji.

Ukaguzi huo umefanyika kwa baadhi ya wateja katika maeneo ya Tabata Kimanga na Kimara Suka jijini Dar es Salaam.

Zoezi hilo lilifanyika Januari 27, 2026, likiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Bi. Irene Gowelle, akishirikiana na timu ya wataalamu.

Lengo la ukaguzi lilikuwa ni kubaini chanzo halisi cha malalamiko na kujiridhisha kuhusu usahihi wa utendaji wa mita za umeme kwa wateja husika.

Matokeo ya vipimo vya kitaalamu yamebaini kuwa mita zote zilizokaguliwa zilikuwa salama na zinafanya kazi kwa usahihi.

Hata hivyo, TANESCO imeeleza kuwa chanzo kikuu cha umeme kuisha haraka ni uchakavu wa wiring za ndani ya nyumba unaosababisha uvujaji wa umeme.

Aidha, matumizi holela ya umeme yameonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa matumizi ya uniti kwa wateja.

Katika nyumba moja Tabata, uchakavu wa wiring ulisababisha upotevu wa takribani uniti mbili za umeme kwa siku, hali iliyoongeza gharama za umeme kwa mteja.

Kwa upande wa Kimara Suka, ilibainika kuwa baadhi ya wateja walikuwa wakitumia umeme bila kuzingatia matumizi bora, ikiwemo kuwasha taa wakati wa mchana.

TANESCO imeendelea kutoa elimu kwa wateja kuhusu matumizi sahihi ya umeme na umuhimu wa kutumia vifaa vyenye ufanisi wa matumizi ya nishati.

Shirika hilo limewataka wananchi wenye changamoto kuwasiliana na TANESCO moja kwa moja kwa ukaguzi na msaada wa kitaalamu badala ya kusambaza taarifa zisizothibitishwa.