…….
Baraza la Wafanyakazi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma limekutana kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za halmashauri pamoja na rasimu ya mapendekezo ya mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo uongozi huo ulieleza kiasi cha bajeti kinachotarajiwa kutekelezwa katika kipindi hicho.
Akizungumza katika kikao hicho, Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Francis Kaunda alisema kuwa halmashauri imekasimia kukusanya shilingi bilioni 166 kutoka vyanzo vyake vya ndani, serikali kuu na wahisani mbalimbali kwaajili ya kutekeleza shughuli za maendeleo, utoaji huduma na kujiendesha.
Kaunda alisema kuwa kutoka mapato ya ndani kiasi cha shilingi bilioni 73 kinatarajiwa kukusanywa ambapo kati ya fedha hizo shilingi bilioni 46 ni mapato yasiyolindwa na shilingi bilioni 27 ni mapato lindwa. Fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida.
Aliongeza kuwa kati ya fedha hizo, kiasi cha shilingi bilioni 32 kimepangwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu, afya na barabara, huku shilingi bilioni 13 zikitengwa kwa matumizi ya kawaida ikiwemo mishahara ya watumishi na uendeshaji wa ofisi. “Msingi wa bajeti hii ni kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kuhakikisha fedha zinapelekwa kwenye vipaumbele vinavyogusa maisha ya wananchi moja kwa moja” Kaunda.
Nae, Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dennis Gondwe alisema kuwa baraza linaunga mkono jitihada za uongozi katika kuandaa bajeti inayozingatia vipaumbele vya maendeleo na maslahi ya watumishi. “Upo umuhimu mkubwa wa ushirikishwaji wa watumishi katika hatua zote za upangaji na utekelezaji wa bajeti ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika kazi. Nawasihi watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuhakikisha malengo ya halmashauri yanafikiwa kwa wakati” alisema Gondwe.
Kwa upande wake, Katibu TALGWU Mkoa wa Dododoma, Audax Stephen aliwataka watumishi kuhakikisha wanafanya usimamizi madhubuti wa fedha za umma na kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya matumizi ya fedha ili kuepuka hoja zisizo za lazima katika ukaguzi. “Tunasisitiza nidhamu ya matumizi ya fedha, uwazi katika manunuzi na uandaaji sahihi wa nyaraka ili kuongeza uwajibikaji na thamani ya fedha” alisema Audax.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi walipata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo yao kuhusu bajeti hiyo, wakisisitiza umuhimu wa kuzingatia maslahi ya watumishi pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili halmashauri iweze kutekeleza mipango yake kwa ufanisi.




