Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Media, Dodoma
Serikali Kuu ya India, kupitia Wizara ya Elektroniki na Teknolojia ya Habari (MeitY), imechukua hatua kali dhidi ya jukwaa la mitandao ya kijamii X (zamani Twitter) kufuatia kusambaa kwa maudhui machafu na ya kudhalilisha wanawake.
Kwa mujibu wa vyanzo vya serikali, X imezuia machapisho 3,500 na kufuta zaidi ya akaunti 600 baada ya serikali kubaini kuwa maudhui hayo yalikuwa yakisambazwa kupitia matumizi mabaya ya zana ya akili bandia iitwayo Grok.
Serikali ilisema watumiaji walikuwa wakitumia Grok kutengeneza na kusambaza picha na video chafu, zikiwemo picha bandia (za kubuniwa na AI) za wanawake, jambo lililokiuka sheria za India na kuhatarisha heshima na usalama wa wanawake na watoto.
MeitY iliipa X muda wa saa 72 kuonyesha hatua ilizochukua na ikaonya kuwa kutotekeleza maagizo hayo kungesababisha hatua kali za kisheria, ikiwemo:
.Kupoteza kinga ya kisheria (safe harbour)
.Kuchukuliwa hatua chini ya Sheria ya TEHAMA
.Mashtaka chini ya sheria za kulinda wanawake na watoto, ikiwemo POCSO
Serikali pia iliitaka X kufanya mapitio ya kina ya mfumo wa Grok, kuweka udhibiti mkali wa maudhui, na kusimamisha au kufuta kabisa akaunti za watumiaji wanaokiuka sheria.
Katika taarifa yake, serikali ilisema kuwa matumizi mabaya ya AI kwa namna hii ni hatari, kinyume cha sheria, na yanaonyesha kushindwa kwa mifumo ya ulinzi ya jukwaa la X.
X imeihakikishia Serikali ya India kuwa itazingatia sheria zote na kuchukua hatua kuhakikisha kuwa maudhui machafu hayaruhusiwi tena kwenye jukwaa Hilo.
Chanzo: NDTV News



