Na John Bukuku – Ikulu, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 itakayofanyika kwa pamoja nchini Tanzania, Kenya na Uganda, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Bw. Reodger Chila Tenga, amesema kuwa maandalizi ya michuano hiyo kwa upande wa Tanzania yanaendelea vizuri, huku dhamira kubwa ikiwa ni kuhakikisha nchi inafanya mashindano yenye viwango vya juu.
Bw. Tenga amesema kuwa mafanikio ya hivi karibuni ya timu ya taifa yameleta faraja kubwa kwa wapenzi wa mpira wa miguu na michezo kwa ujumla, akieleza kuwa vijana wamepambana kwa juhudi kubwa na kufanikiwa kuvunja rekodi za miaka ya nyuma kwa kupata pointi ambazo hazijawahi kupatikana hapo awali, licha ya kukutana na timu ngumu.
Aidha, amebainisha kuwa mchango wa wachezaji pamoja na benchi la ufundi umekuwa mkubwa na unaojenga imani kwa siku zijazo, hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania inajiandaa kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya Afrika. Amesema kuwa matarajio ya wadau wa michezo ni kuona timu ikiendelea kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo.
Bw. Tenga amesema kuwa mafanikio hayo yameongeza matumaini na furaha kwa Watanzania wengi, akisisitiza kuwa heshima iliyopatikana ni matokeo ya juhudi na kujituma kwa wanamichezo hao. Aidha, amebainisha kuwa Serikali imeendelea kufanya kazi kubwa katika kuimarisha mazingira ya michezo nchini.
Katika maandalizi ya AFCON 2027, amesema kuwa kazi kubwa tayari imefanyika na kinachohitajika kwa sasa ni kukamilisha maandalizi kwa ufanisi. Amebainisha kuwa mashindano hayo yatakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha kiwango cha mpira wa miguu, kuhamasisha michezo kwa ujumla, kuimarisha ushirikiano wa nchi shiriki pamoja na kuitangaza Tanzania kimataifa.
Bw. Tenga amesema kuwa mafanikio ya mashindano hayo hayatategemea Wizara ya Michezo au Serikali pekee, bali yanahitaji ushiriki wa kila Mtanzania wakiwemo wananchi wa kawaida, wafanyabiashara na wapenzi wa michezo, ili kuhakikisha AFCON 2027 inafanyika kwa mafanikio makubwa na yenye heshima kwa taifa.



