Na John Bukuku – Ikulu Dar es Salaam
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, amesema kuwa lengo kuu la Taifa Stars ni kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya kimataifa na kuiletea heshima Tanzania, hususan kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika nyumbani mwaka 2027.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa chakula cha mchana alichoandaliwa timu ya Taifa Stars Januari 10, 2026, amesema kuwa Serikali imeendelea kutoa rasilimali zote muhimu pamoja na kujenga miundombinu itakayosaidia mashindano ya kimataifa yatakayofanyika mwakani katika nchi tatu ikiwemo Tanzania.
Aidha, amebainisha kuwa TFF imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha karibuni kwa kuacha changamoto za nyuma na kuelekeza nguvu katika maendeleo ya soka la vijana pamoja na timu za taifa.
Amesema kuwa Tanzania imefanikiwa kufuzu kushiriki Mashindano ya Dunia ya wasichana chini ya umri wa miaka 17, hatua inayodhihirisha ukuaji wa mpira wa miguu wa wanawake nchini.
Aidha, amebainisha kuwa katika Mashindano ya Afrika ya wasichana chini ya miaka 15 yaliyofanyika Durban mwaka 2023, Tanzania iliibuka mabingwa, huku mwaka uliofuata timu ya wavulana chini ya miaka 15 ikitwaa ubingwa wa Afrika Mashariki katika mashindano yaliyofanyika Zanzibar mwaka 2024.
Amesema kuwa mwaka 2025, katika mashindano yaliyofanyika Accra, Ghana, vijana wa Kitanzania chini ya miaka 15 walifanikiwa kutwaa ubingwa wa Afrika kwa mara ya pili mfululizo.
Aidha, amebainisha kuwa timu za wavulana na wasichana chini ya miaka 15 zimefanikiwa tena kufuzu kushiriki Mashindano ya Afrika yatakayofanyika nchini Nigeria mwaka huu.
Amesema kuwa vijana hao wote walipatikana kupitia zoezi la usaka vipaji (skauti) lililofanyika nchi nzima na kupelekwa katika Kituo cha Maendeleo cha TFF kilichopo Tanga Nyanjani, ambacho kimekuwa chanzo kikuu cha mafanikio hayo.
Aidha, amebainisha kuwa kutokana na mafanikio hayo, kituo hicho kimepandishwa hadhi na kuwa Academy rasmi, itakayozinduliwa mwaka huu na Rais wa FIFA, Gianni Infantino.
Amesema kuwa Rais wa FIFA ameonesha nia ya kushiriki uzinduzi huo sambamba na uwepo wa Rais Samia Suluhu Hassan, mara baada ya kupatikana kwa tarehe itakayofaa.
Aidha, amebainisha kuwa timu ya Taifa ya wanawake, Twiga Stars, imepata mafanikio makubwa ikiwemo kutwaa ubingwa wa CECAFA Challenge, kushiriki AFCON iliyofanyika Morocco mwaka 2025 na kupanda nafasi nane katika viwango vya FIFA kupitia mradi wa kimataifa wa MZUKA.
Amesema kuwa timu ya Serengeti Boys chini ya miaka 17 imefanikiwa kutwaa ubingwa wa CECAFA kwa mara ya pili mfululizo na kufuzu kushiriki AFCON ya U-17 itakayofanyika nchini Congo, ikiwa na lengo la kufuzu Kombe la Dunia.
Aidha, amebainisha kuwa timu ya wasichana chini ya miaka 20 imebakiza mechi moja ya mwisho dhidi ya Kenya katika hatua ya kufuzu, na endapo itapata ushindi itashiriki Kombe la Dunia.
Amesema kuwa mafanikio hayo yametokana na sapoti kubwa kutoka Serikalini, Wizara ya Michezo pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
Aidha, amebainisha kuwa katika mashindano ya AFCON yaliyofanyika Morocco, Ligi Kuu ya Tanzania ilishika nafasi ya nne kwa kutoa idadi kubwa ya wachezaji.
Pia amesema kuwa TFF itaendelea kutumia sapoti inayopatikana kutoka Serikalini kuhakikisha Taifa Stars na timu nyingine za taifa zinafanya vizuri zaidi, huku matarajio makubwa yakiwekwa kuelekea mashindano ya AFCON yatakayofanyika nyumbani mwaka 2027.




