Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Media, Dodoma
Klabu ya Manchester City imekamilisha rasmi usajili wa mshambuliaji Antoine Semenyo kutoka AFC Bournemouth baada ya kufikia kifungu cha kuvunja mkataba wake chenye thamani ya pauni milioni 65.
Semenyo, mwenye umri wa miaka 26, amesaini mkataba wa muda mrefu wa miaka mitano na nusu utakaomuweka ndani ya Etihad Stadium hadi mwaka 2031. Usajili huo unaufanya kuwa wa kwanza kwa Manchester City katika dirisha hili dogo la usajili.
Man City wamewashinda wapinzani wao wakubwa Manchester United, Liverpool, Tottenham Hotspur na Chelsea, ambazo pia zilikuwa zikihitaji saini ya mshambuliaji huyo kutokana na kiwango chake bora msimu huu.
Mshambuliaji huyo aliyezaliwa London lakini anayoiwakilisha Ghana kimataifa kupitia urithi wa baba yake, amekuwa katika kiwango cha juu akiwa na Bournemouth baada ya kufunga mabao 10 na kutoa pasi 3 za mabao katika michezo 20 ya Ligi Kuu ya England msimu huu.
Safari ya Semenyo katika soka haikuwa rahisi, kwani aliwahi kukataliwa na klabu za Arsenal, Tottenham na Millwall alipokuwa kijana. Baadaye alijiunga na akademi ya West Country chini ya mfumo uliowahi kusimamiwa na kocha wa zamani wa Leeds United na Forest Green Rovers, Dave Hockaday, kabla ya kujijengea jina kupitia Bristol City na kisha Bournemouth.
Manchester City inategemea usajili wa Semenyo kuongeza nguvu na ushindani katika safu ya ushambuliaji chini ya kocha Pep Guardiola, hasa katika kipindi ambacho klabu hiyo inapigania mataji ya ndani na Ulaya.
Kwa upande wa Bournemouth, mauzo ya Semenyo ni pigo kubwa kiufundi, lakini yanawapa faida kubwa kifedha huku yakithibitisha uwezo wao wa kukuza na kuuza vipaji katika soka la England.




